2017-07-01 16:38:00

Prof. Don Giuseppe Costa ang'atuka kutoka Idara ya Uchapishaji, LEV


Askofu mkuu Angelo Becciu, Katibu mkuu msaidizi wa Vatican, Ijumaa, tarehe 30 Juni 2017 amemshukuru na kumpongeza sana Professa Don Giuseppe Costa, SDB ambaye kwa muda wa miaka kumi amejisaka bila ya kujibakiza kama Mkurugenzi mtendaji wa Kituo cha Uchapaji cha Vatican, LEV na kwa sasa amemaliza muda wake. LEV ni kituo muhimu sana kinachochapisha shughuli zote za Vatican na kwamba, kwa sasa Don Costa anarejea tena Shirikani kwake kuendelea na maisha na utume wake wa kitawa! Kabla ya kuagwa rasmi, alipata bahati ya kuandikiwa baraua binafsi, kukutana na kuagana na Baba Mtakatifu Francisko ambaye amemshukuru na kumpongeza kwa jitihada zake za kueneza na kudumisha utamaduni wa Kikristo na Mafundisho ya Kanisa

Katika salam zake za utangulizi, Monsinyo Dario Edoardo Viganò, Mwenyekiti wa Sekretarieti ya Mawasiliano mjini Vatican amesema, Kituo cha Uchapishaji cha Vatican kitakuwa ni sehemu ya Sekretarieti ya Mawasiliano mjini Vatican kama sehemu ya utekelezaji wa mageuzi yanayofanywa na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican. Hafla ya kumuaga Don Costa imehudhuriwa na viongozi mbali mbali kutoka Sekretarieti kuu ya Vatican pamoja na wanashirika la Wasalesiani wa Don Bosco na Gazeti la L’Osservatore Romano ambalo pia liko kwenye mchakato wa mabadiliko kuhusu vyombo vya mawasiliano ya jamii mjini Vatican.

Katika kipindi cha miaka 10 iliyopita, Don Costa amefanya maboresho makubwa katika Kituo cha Uchapaji cha Vatican, LEV na kwamba, haya ni matunda ya juhudi, maarifa, weledi, bidii na ugunduzi uliomwilishwa katika maisha na utume katika kipindi chake cha uongozi. Ni mtawa ambaye amejisadaka sana kwa ajili ya huduma kwa Kanisa amekaza kusema, Askofu mkuu Becciu ambaye pia amewapongeza wafanyakazi wote wa LEV kwa majitoleo yao na kwamba, juhudi za makusudi hazina budi kufanya ili hatimaye, kuhakikisha kwamba, sauti ya Khalifa wa Mtakatifu Petro iweze kusikika na hatimaye kupendwa.

Professa Don Giuseppe Costa, SDB ni mtaalam aliyebobea katika masuala ya uandishi na uchapaji wa vitabu, kwa miaka kadhaa amekuwa ni Jalimu wa Uandishi wa Habari, Chuo Kikuu cha Wasalesiani, mjini Roma. Kwa upande wake, amechukua fursa hii kuonesha furaha inayobubujika kutoka katika sakafu ya moyo wake kwa kuwezeshwa kupata nafasi ya kushirikisha karama namapaji yake; katika hali ya unyenyekevu na kwa kutambua kwamba, katika hali kama hii inawezekana pia kufanya mambo makuu.

Ni matumaini yake kwamba, Sekretarieti ya Mawasiliano mjini Vatican itaendelea kufanya maboresho katika huduma zinazotolewa na LEV ili kuwafanikia watu wengi zaidi. Professa Don Giuseppe Costa, SDB alizaliwa kunako mwaka 1946 huko Messina, Kusini mwa Italia, akapewa Daraja Takatifu ya Upadre kunako mwaka 1974. Alijipatia Shahada yake ya uzamivu katika masuala ya uandishi wa habari huko Marekani na kwa miaka mingi amefundisha somo la nadharia na vitendo katika uandishi wa habari, Chuo kikuu cha Kipapa cha Wasalesiani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.