2017-06-30 07:00:00

Mchango wa Kanisa kujenga dunia yenye umoja na amani kupitia elimu


Kanisa katoliki linao uzoefu wa karne na karne katika kutoa elimu na kuwaandaa kimalezi sio tu wakatoliki, bali vijana wote wa kike na wa kiume, wa madhehebu na dini mbali mbali, ambao wanapata fursa hiyo kupitia taasisi mbali mbali za elimu zilizoanzishwa na zinazosimamiwa na Kanisa katika kila kona ya dunia. Askofu mkuu Bernadirto Auza, Mwakilishi wa Kudumu wa Vatican kwenye Umoja wa Mataifa, siku ya Jumatano tarehe 28 Juni 2017, akichangia hoja juu ya upatikanaji wa elimu bora kwa wote katika kufikia malengo ya maendeleo endelevu, ameonesha ni jinsi gani Kanisa linatoa mchango mkubwa katika kujenga dunia yenye umoja na amani kwa kutumia elimu.

Baba Mtakatifu Francisko, akihutubia Mkutano mkuu wa Umoja wa Mataifa mnamo 2015 alisema: haki elimu, ni haki inayopaswa kuzingatiwa kwanza kabisa kutoka kwenye familia na kwa jamii za kidini katika kuchangia elimu na malezi bora ya watoto na vijana. Huu utakuwa msingi wa utekelezaji wa Ajenda ya maendeleo endelevu kufikia 2030. Askofu mkuu Bernadirto Auza anasema, ili kufanikisha wajibu huo ni lazima kujega utamaduni wa kukutana. Utamaduni huu unapaswa ujengeke katika heshima, thamani kwa wengine, majadiliano, usikilizaji, na mshikamano, bila kudharau utambulisho wa mwengine. Hatua hii itakuwa ni nyenzo ya kupiga vita ghasia, ubaguzi, umaskini, unyonyaji, na uonevu.

Taasisi za elimu, ziwajengee uwezo vijana kutafuta suluhu za changamoto kwa kujikita kwenye majadiliano ya pamoja, yanayosimikwa kwenye misingi ya ukweli, uwazi, haki na weledi. Hivi karibuni Baba Mtakatifu Francisko alifungua Ofisi za Scholas Occurentes Foundation mjini Vatican. Scholas Occurentes Foundation ni mfuko ulioanzishwa na Baba Mtakatifu Francisko mwaka 2013, unaohusika na mashule kwenye nchi takribani 190 duniani, kwa lengo la kuwajengea uwezo vijana kuwa na utamaduni wa kukutana na kujadiliana katika fani za elimu, teknolojia, sanaa na michezo. Wakati wa ufunguzi wa ofisi zao mjini Vatican, Baba Mtakatifu alitoa tahadhari ya kutokujenga tabaka la wasomi.

Askofu mkuu Bernadirto Auza anasisitiza kwamba elimu isionekane kuwa ni upendeleo kwa ajili ya wenye fedha tu, bali iwe fursa kwa wote duniani kwani elimu inapanda matumaini, na matunda yake ni upatikanaji wa ukweli, uelewa, weledi, wema, umakini, unadhifu na mshikamano kati ya vizazi. Hivyo wakufunzi na walezi wanapowasikiliza wanafunzi na wanafuzni kuwasikiliza walezi wao, dunia yenye umoja na amani itaanza kuchukua mkondo wake.

Padre Celestine Nyanda.

Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.