2017-06-29 14:21:00

Katika mateso Kristo yupo pamoja na waamini


Mababa wa Kanisa walipenda kuwaita Watakatifu Petro na Paulo kuwa ni mihimili ya Kanisa, ambapo ujenzi wa Kanisa la Kristo umesimikwa. Wote wawili walimwaga damu yao kwa ajili ya ushuhuda kwa Kristo, baada ya safari na mahangaiko mengi ya kuitangaza Injili ya Kristo na huduma kwa Kanisa la awali lililokuwa linakua. Ni kwa sababu hiyo, imani yao walioikiri na walioitangaza kishujaa, imevikwa taji la heshima kwa ufiadini wao. Baba Mtakatifu Francisko, kwa namna hiyo ameanza kuusalimu umati wa waamini waliokusanyika katika uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, wakati wa sala ya Malaika wa Bwana, siku ambapo Kanisa linaadhimisha sikukuu ya Watakatifu Petro na Paulo.

Mtume Petro alishuhudia uhasama dhidi ya Injili ya Bwana, uhasama uliopelekea yeye mwenyewe kutiwa gerezani na Mfalme Herode ili aje ahukumiwe baadae, lakini aliokolewa kwa namna ya miujiza ili aweze kuendelea kuitangaza Injili kuanzia nchi Takatifu na baade Roma, akizitumia nguvu zake zote kwa ajili ya huduma kwa jumuiya ya kikristo. Mtume Paolo pia alipitia chuki na uhasama mwingi kutoka kwa watawala kisiasa na kidini enzi za Dola ya kirumi, lakini Bwana alimwezesha kuitangaza Injili kwa wapagani na kufungua jumuiya nyingi za kikristo kati yao.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, kuokolewa huko kimiujiza kwa Miamba ya Kanisa, Petro na Paulo, ni ishara kwamba Bwana yupo na waamini, yupo na Kanisa siku zote, hawaachi yatima bali anawasindikiza katika maisha yao ya kila siku wanapoitangaza na kuishuhudia Injili yake. Katika mahangaiko yote, waamini wasikate tamaa, wamwamini Mungu ambaye anao uwezo wa kuwatoa katika mitego yote ili waendelee kumtolea ushuhuda. Hata hivyo waamini wawe makini sana na adui namba moja, ambaye ni dhambi. Shetani anamshawishi mwamini atende dhambi na kujitenga na nguvu ya Kristo, nguvu pekee iwezayo kumuokoa. Hivyo inapotokea wanaanguka dhambini, mara moja wajipatanishe katika Sakramenti ya Kitubio, ili waendelee kuipeperusha bendera ya ushindi dhidi ya dhambi.

Baada ya sala ya Malaika wa Bwana, Baba Mtakatifu kaendelea kuonesha ukaribu wake wa kibaba kwa makardinali watano wapya na maaskofu wakuu 36 waliopokea Pallio Takatifu. Kautambua pia uwepo wa ujumbe wa Patriak wa kiekumene Bartolomeo I, ambao ni ishara ya kudumu ya umoja na udugu kati ya makanisa.

Na Padre Celestine Nyanda

Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican.

 

 

 

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.