2017-06-27 08:07:00

Papa Francisko asema, umoja, mshikamano na ushuhuda ni muhimu sana!


Baba Mtakatifu Francisko amemwandikia barua Patriaki Youssef Absi aliyechaguliwa hivi karibuni kuwa Patriaki mpya wa Kanisa la Kigiriki la Kikatoliki huko Antiokia na Mashariki yote, akionesha uwepo wake wa karibu na mshikamano. Baba Mtakatifu anasema, amepokea kwa furaha kubwa barua kutoka kwa Patriaki Youssef Absi ya kuomba kuwa na umoja wa Kikanisa na Khalifa wa Mtakatifu Petro. Anapenda kumhakikishia uwepo wa karibu kwa njia ya sala, ili Kristo Yesu, mchungaji mwema aweze kumsimamia katika maisha na utume wake aliokabidhiwa kwa ajili huduma kwa familia ya Mungu.

Baba Mtakatifu anasema, uchaguzi wa Patriaki Youssef Absi unakuja ambapo Kanisa linakabiliwa na hali ngumu huko Mashariki ya Kati; changamoto inayowaalika Wakristo kutangaza na kushuhudia kwa ari na moyo mkuu, imani yao kwa Yesu Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Katika kipindi hiki kigumu cha mateso, dhuluma na nyanyaso dhidi ya Wakristo, viongozi wa Kanisa kwa namna ya pekee kabisa wanatakiwa kuonesha umoja, mshikamano, ukaribu, ukweli, uwazi na uaminifu mbele ya familia ya Mungu inayoteseka kwa wakati huu!

Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, Patriaki Youssef Absi akiwa ameungana na Mababa wa Sinodi, katika hekima na busara ya Kiinjili ataweza kuwa ni Baba na kiongozi mkuu katika huduma kwa waamini wa Kanisa la Kigiriki la Kikatoliki huko Antiokia na Mashariki yote, lakini zaidi kama shuhuda mwaminifu wa Kristo Mfufuka. Kwa dhamana aliyopewa kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, Baba Mtakatifu Francisko anasema, anapenda kumpatia umoja wa Kikanisa mintarafu Kanuni na Sheria za Kanisa la Mashariki. Anapenda kumzamisha katika ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa Mungu kwa kumpatia baraka zake za kitume ambazo anapenda pia ziwafikie viongozi wa Kanisa na waamini wote katika ujumla wao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.