2017-06-27 13:42:00

Matumizi haramu ya dawa za kulevya yanaangamiza Jumuiya ya Binadamu


Siku ya kimataifa ya kupiga vita matumizi haramu ya dawa za kulevya, iliyowekwa na Umoja wa Mataifa, ni fursa muhimu kukumbusha dhamiri za watu kwamba biashara ya dawa za kulevya inazidi kushamiri sana katika mifumo mbali mbali ikisindikizwa na uhalifu wa namna nyingine dhidi ya utu wa binadamu. Hivi ndivyo Kardinali Peter Turkson, Mwenyekiti wa Baraza la kipapa kwa ajili ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu, anaanza kutoa ujumbe wake wa mwaka 2017, kwa siku ya kimataifa dhidi ya dawa za kulevya.

Leo hii matumizi ya dawa za kulevya yanaonekana kuwa ni mahitaji ya kila siku kwa ajili ya starehe, na wakati mwingine kama hitaji kwa ajili ya kujiweka vizuri. Mbali ya "Cocain" na "Heroin", kuna dawa zingine za kulevya zinazosemekana kupatikana kwa bei nafuu kidogo na kuvutia wengi walio kwenye magumu mbali mbali ya maisha, wakiamini kwamba zitawapa unafuu. Kati ya zote, Bangi inaonekana kutumika zaidi. Kuna umuhimu wa kufahamu madhara yake kwa kina na kuweka sera za kudhibiti matumizi yake katika nchi mbali mbali, anasema Kardinali Turkson. Sheria za udhibiti wa dawa za kulevya zinatofautiana nchi kwa nchi, lakini kuna haja ya kutafuta suluhu za dharura na kwa haraka ili kuhakikisha unapatikana ufumbuzi wa kudumu. Mikakati ya kupambana dhidi ya biashara ya dawa za kulevya inapaswa kulenga sio tu kupunguza madhara, bali ni muhimu kuzingatia matumizi yake halali kwa kiwango halali.

Katika kuzingatia matumizi halali hasa Hospitalini, umakini uwekwe kuepuka kusababisha athari za dawa hizo kiakili kwa wagonjwa, na kuwafanya wawe tegemezi baada ya matibabu. Ni wazi kwamba utegemezi wa dawa za kulevya unasababishwa na vitu vingi, ikiwa ni pamoja na upweke, makuzi yasiyofumbatwa na tunu bora kifamilia, pamoja na matatizo ya kijamii. Hivyo kila mwathirika wa dawa za kulevya atambuliwe kwa historia yake, apendwe na kusaidiwa kadiri inavyowezekana. Watu wote wenye mapenzi mema, washirki kikamilifu katika kutengeneza sera na mipango mikakati kupiga vita biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya. Kati ya mbinu zenye mafanikio ni pamoja na utoaji wa elimu kuhusu dawa za kulevya, hasa kwa vijana wa kizazi kipya. Wana taaluma katika jamii, watengeneze mfumo mzuri wa kuelimisha watu kwa namna ambayo ni endelevu, na sio kuchukuliwa kana kwamba ni jambo la msimu.

Kardinali Turkson anasisitiza kwamba, wazazi na walezi, wazingatie malezi yanayomjenga kijana katika tunu msingi na maadili mema ndani ya jamii, kiasi cha kuwa na uwezo wa kukubali uhalisia wa maisha na kukabiliana nao katika changamoto zake, badala ya kutafuta njia za mkato za kuwa na furaha za msimu ambazo zina madhara makubwa kwa mtu binafsi na kwa jamii kwa ujumla. Uhai na maisha ni zawadi yenye thamani kubwa, ambayo mwanadamu anapaswa kuiheshimu badala ya kukwepa kwa kutafuta hifadhi kwenye kivuli cha dawa za kulevya.

Baba Mtakatifu Francisko anasema: vijana wanahitaji kizunguzungu fulani kinachowafanya wajisikie wachangamfu, kizunguzungu kama changamoto ya kuwafanya wazibadili ndoto zao ziwe miradi katika fani mbali mbali. Vijana wasaidiwe kufikia malengo yao, kwa kuwawezesha kuwa washiriki wakuu wa kujenga maisha yao. Wasipopata kizunguzungu hicho kutoka kwa watu makini, vijana wataangukia kwenye mikono ya watu wasiojielewa na kuwapoteza.

Kardinali Peter Turkson anaalika jamii ya leo kuwafunda vijana kuishi kwa upendo na furaha katika familia na jumuiya mbalimbali, kwa kuwa na utamaduni wa kujali usafi binafsi. Maisha ya kiroho yawe dira katika kutafuta maana na umuhimu wa zawadi ya maisha. Matumizi na utegemezi wa dawa za kulevya utaharibu sana jumuiya ya binadamu, kwani mtu asipojipenda na kujijali mwenyewe, hawezi kupenda na kujali jirani yake. Vijana wajengewe utamaduni wa kukutana na kujenga urafiki kati yao badala ya kuendekeza maisha ya upweke na ubinafsi.

Na Padre Celestine Nyanda.

Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican.

 

 

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.