2017-06-27 13:58:00

Kardinali Nichols ahutubia Bunge la Lithuani dhidi ya utumwa mamboleo


Kardinali Vincent Nichols, Rais wa kikundi cha Mtakatifu Martha akizungumza katika Bunge la Lithuania, amewatia moyo wajumbe wa bunge hilo katika mapambano yao dhidi ya biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo. Kikundi cha Mtakatifu Martha ni kikundi cha kimataifa, kilichoanzishwa mwaka 2014 na Baba Mtakatifu Francisko kwa lengo la kupambana na biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo. Kikundi hicho kinashirikiana na majimbo, jeshi la polisi, maafisa wa uhamiaji katika nchi 36 kwa sasa, ili kuhamasisha uelewa wa pamoja wa mapambano hayo na kuwasaidia walioathirika kwa biashara hiyo.

Kikundi cha Mtakatifu Martha kina mapadri walezi, madaktari na wana sheria wa kujitolea wanaohangaika usiku na mchana kwa ajili ya kuwahudumia waathirika wa biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo, ili kuwarejeshea afya zao na kutetea haki zao msingi. Jijini London kunafunguliwa chuo kikuu cha Mt. Maria, kwa ajili ya mafunzo ya namna ya kupambana na biashara hiyo haramu. Ushirikiano kati ya kikundi cha Mtakatifu Martha na serikali mahalia, umeleta mafanikio makubwa katika nchi za Nigeria, Msumbiji, Argentina na Irland.

Kardinali Vincent Nichols anaelezea kwamba, Kanisa linapambana na bishara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo, sababu ni kinyume kabisa na heshima kwa utu wa binadamu, ambao unapaswa kulindwa kwa kila binadamu na kwa kila wakati bila kutafuta visingizio vya kukwepa wajibu huo. Heshima kwa utu wa binadamu haubaguliwi kwa kufuata nafasi katika jamii au uwezo wa mtu, bali inaambatana na ukweli wa uwepo wa binadamu, aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, zawadi ambayo Mwenyezi Mungu mwenyewe anaiheshimu, kwani Yeye ni Baba wa wote.

Biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo ni dhihaka na kashifa kubwa dhidi ya heshima kwa utu wa binadamu. Kuna watu zaidi ya milioni 20 leo wamenaswa kwenye utumwa mamboleo. Ni uovu uliooza na unamwangamiza mwanadamu, aibu ambayo haiwezi kufutwa kwa maneno tu bali kwa kupambana kuitokomeza kwenye uso wa dunia. Kardinali Nichols amempongeza sana Kamishina Kevin Hyland kwa kuhangaikia vita dhidi ya biashara haramu ya binadamu kuwa moja ya malengo endelevu ya Umoja wa Mataifa. Kikundi cha Mt. Martha kinanuia kumrudishia hali nzuri kila mwathirika wa utumwa mamboleo, kwani mwathirika ndiye anapaswa kupewa kipaumbele. Lakini pia kuongeza nguvu kwenye utawala wa sheria, kuvunjilia mbali mtandao wa uhalifu, kisha kutiwa nguvuni na kushitakiwa kwa wahalifu wa biashara hiyo.

Shughuli hizi zote zinategemea sana suala la msingi ambalo ni uaminifu. Uaminifu huchukua muda kuujenga na bidii kubwa huhitajika katika kuudumisha. Hata hivyo uaminifu na kuaminiana kukishajengeka, hutoa fursa nzuri ya ushirikiano kati ya vyombo vya usalama na Kanisa kutenda kwa weledi na kupata mafanikio makubwa. Kwa upande wa Kanisa, ni msukumo wa kujali na kuhangaikia wanyonge, hali kwa upande wa vyombo vya usalama ni kazi yao kutokomeza uhalifu na kuwawajibisha kisheria wanaovunja sheria. Utendaji wa ushirikiano namna hii huwa na mchango mkubwa sana katika kutafuta mafao ya wengi, anasema Kardinali Nichols.

Baada ya hotuba yake kwa Bunge la Lithuani, Kardinali Vincent Nichols alikutana na Waziri mkuu wa Lithuani Bwana Saulius Skvernelis, Waziri wa mambo ya ndani Bwana Eimutis Misiunas. Akiwa nchini Lithuani, Kardinali Nichols, siku ya Jumapili, tarehe 25 Juni 2017, alipata fursa ya kushiriki Misa Takatifu ya kumtangaza Askofu mkuu Teofilius Matulionis kuwa Mwenyeheri, Ibada iliyoongozwa na Kardinali Angelo Amato, Mwenyekiti wa Baraza la kipapa la kuwatangaza waamini kuwa Wenyeheri na Watakatifu.

Na Padre Celestine Nyanda.

Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican.

 

 

 

 

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.