2017-06-27 07:30:00

Hatari ya habari za kughushi!


Nchini Ufilippini hivi karibuni kumekuwa na habari kadhaa ambazo zimetolewa na vyombo vya habari kwa namna ambayo siyo sahihi, yaani hazikuakisi ukweli wa habari husika. Habari hizo za kugushi zimepelekea mgawanyiko kati ya watu, ukosefu wa imani kwa viongozi wa serikali, zimejenga chuki dhidi ya serikali, na kusababisha ghasia baadhi ya maeneo. Baraza la Maaskofu nchini Ufilipini limekemea tabia hiyo ya vyombo vya habari kupindisha ukweli wa habari na kusababisha mkanganyiko na mgawanyiko kati ya raia wa Ufilippini. Askofu mkuu Socrates Villegas, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Ufilippini anasema: kila mmoja aepuke kabisa kusaidia utengenezwaji, kutetea, au kusambaza habari ambazo hana uhakika nazo, au hata anafahamu wazi kuwa sio za kweli au sio kamili na zina lengo la kuvuruga amani, umoja, udugu na mshikamano wa wananchi wa Ufilippini.

Kusambaza taarifa zisizo za kweli ni dhambi dhidi ya ukarimu, sababu inazuia watu kufanya maamuzi sahihi na yenye kujenga, badala yake wanachukua maamuzi yenye makosa ambayo hupelekea kuvuruga jamii ya watu, wanasema Maaskofu nchini Ufilippini. Ushiriki hai wa raia katika kujenga jamii ya haki, unategemea sana maisha yanayofumbatwa katika kweli, na sio habari za kugushi. Katika nchi ya Ufilippini, asilimia hamsini na nane (58%) kati ya raia milioni sitini (60) wanatumia internet. Maaskofu nchini humo, wanawaasa raia kuchunguza ukweli wa habari zinazosambazwa katika mitandao jamii. Tangu kuchaguliwa kwa Bwana Rodrigo Duterte mwaka 2016, kuwa Rais wa nchi ya Ufiliipini, kumekuwa na tabia za kuwachafua kwa njia ya mitandao, wale wanaokosoa utawala wa serikali hiyo.

Na Padre Celestine Nyanda.

Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican.

 

 

 

 

 

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.