2017-06-27 15:11:00

Cheche za matumaini: Miaka 50 ya mchakato wa majadiliano ya kiekumene


Katika maadhimisho ya Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo, miamba wa imani, kumekuwepo na utamaduni wa uwepo wa wawakilishi kutoka katika Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli, kama sehemu ya mchakato wa kukuza na kudumisha majadiliano ya kiekumene katika maisha ya sala. Hata katika maadhimisho ya Sherehe ambayo inaadhimishwa na Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 29 Juni, Patriaki Bartolomeo wa kwanza akiwa ameungana na Sinodi ya Mashariki, ametuma ujumbe mjini Vatican ili kushiriki katika sherehe. Wajumbe hawa wamekutana na Baba Mtakatifu Francisko, Jumanne, tarehe 27 Juni 2017.

Baba Mtakatifu katika hotuba amekaza kusema, Petro na Paulo ni mitume wa Kristo waliojisadaka na kumtumikia Kristo kwa njia tofauti; wakawa ni mashuhuda na vyombo vya upendo wa huruma ya Mungu, kila mtu kwa nafasi na kadiri alivyowezeshwa na Mwenyezi Mungu, kiasi hata cha kuyamimina maisha yao; tukio linalowaunganisha wote na Makanisa yote yanaadhimisha sherehe katika umoja na mshikamano. Hiki ni kielelezo cha umoja katika utofauti ndani ya Kanisa; hali ambayo inapaswa kudumishwa.

Uwepo wa wawakilishi kutoka Kanisa la Kiorthodox na Kikatoliki ni juhudi za Makanisa haya mawili kutaka kujenga na kudumisha umoja; udugu sanjari na uekumene wa sala na huduma ya Injili, changamoto kubwa ni kwa Makanisa haya mawili kujielekeza katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi, chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa, kwa kuendelea kutunza na kudumisha amana ya ukweli na imani.  Ni wajibu wa Makanisa haya mawili kuendeleza Mapokeo ya Kitaalimungu, Maisha ya kiroho na Sheria za Kanisa mintarafu Mafundisho ya Mitume na Mitaguso wa Kiekumene, kama chemchemi rejea katika mchakato wa ujenzi wa umoja kamili wa Kanisa, umoja unaosimikwa katika utofauti!

Makanisa haya mawili anasema Baba Mtakatifu Francisko yanaadhimisha kumbu kumbu ya Miaka 50 tangu Mwenyeheri Paulo VI alipokutana, kusali na kuzungumza na Patriaki Athenagoras mjini Phanar, Julai 1967 na baadaye wakakutana tena mwezi Oktoba, 1967 mjini Roma. Viongozi hawa wawili walisukumwa na upendo wao kwa Kanisa, ili kuanza hija ya kiekumene, ili siku moja Makanisa haya mawili yaweze kufikia umoja kamili, changamoto ambayo inapaswa kuendelea kuvaliwa njuga na Makanisa kwa wakati huu. Uwepo wa wawakilishi kutoka Kanisa la Kiorthodox ni ushuhuda wa furaha iliyooneshwa na Wakristo miaka 50 iliyopita! Tangu wakati huo, kumekuwepo na uwakilishi wa Makanisa katika maadhimisho ya Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo pamoja na Mtakatifu Andrea msimamizi wa Kanisa la Costantinopoli.

Baba Mtakatifu anamshukuru na kumpongeza kwa namna ya pekee kabisa Patriaki Bartolomeo wa kwanza ambaye walibahatika kukutana tena hivi karibuni wakati wa hija yake ya kitume nchini Misri. Huko ameshuhudia umuhimu wa kushikikamana na kuwa na msimamo mmoja ili kukabiliana na changamoto mbali mbali katika maisha na utume wa Kanisa na katika ulimwengu mamboleo! Mwezi Septemba, 2017 huko Leros, Ugiriki kutafanyika mkutano wa Kamati ya Uratibu ya Tume ya Pamoja ya Kiekumene Kimataifa ya Majadiliano ya Kitaalimungu kati ya Kanisa Katoliki na Kanisa la Kiorthodox, inayosimamiwa na Mwenyekiti mwenza Kardinali Kurt Koch kwa mwaliko wa Askofu mkuu Paisios.

Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, mkutano huu utafanyika katika mazingira ya utulivu wa maisha ya kiroho, kwa kutambua na kuthamini safari ya kiekumene iliyokwisha kufanyika hadi wakati huu baina ya Makanisa haya mawili, ili kuendeleza zaidi majadiliano ya kiekumene, ili kumwilisha ile sala ya Kristo Yesu kabla ya mateso yake, ili wote wawe wamoja. Dhamana hii inahitaji unyenyekevu na utii. Baba Mtakatifu amehitimisha hotuba yake kwa kuyaombea Makanisa haya ulinzi na tunza ya Watakatifu Petro, Paulo na Andrea, Mitume, ili waweze kuwasaidia kuwa ni vyombo vya umoja na amani duniani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.