2017-06-26 14:49:00

Zijengeeni familia uwezo wa kupambana na ugonjwa wa saratani!


Shirikisho la Mapambano ya Saratani Kitaifa nchini Italia, LILT, ni utajiri mkubwa unaoiwezesha Italia kuwaunda watu na familia katika mchakato wa kuzuia kuenea kwa ugonjwa wa saratani, kwa kuwa na maisha bora zaidi. Ni shirikisho linalosaidia kuchochea tabia ya watu kujitolea kuwasaidia jirani zao katika uhalisia wa maisha ya kila siku! Kuna haja ya kuendelea kujikita katika ujenzi na ukuzaji wa utamaduni wa maisha unaofumbatwa katika tabia na mwenendo wa maisha.

Haya yamesemwa na Baba Mtakatifu Francisko alipokutana na kuzungumza na wanachama wa Shirikisho la Mapambano ya Saratani Kitaifa nchini Italia, Jumatatu, tarehe 26 Juni 2017. Kuna haja ya kuzisindikiza familia na kuwasaidia watu wengi zaidi kufumbata utamaduni wa uhai dhidi ya matamanio ya kibiashara. Familia zijengewe uwezo wa kuzuia ugonjwa wa Saratani, dhamana inayopaswa kuvaliwa njuga na wadau kutoka katika vizazi mbali mbali, ili kujenga na kuimarisha mafungamano ya kijamii yanayozingatia uzoefu na mang’amuzi ya waathirika wa ugonjwa wa Saratani pamoja na familia zao, changamoto pevu katika kukabiliana na ugonjwa wa Saratani!

Baba Mtakatifu Francisko anawapongeza na kuwashukuru wanachama wa Shirikisho la Mapambano ya Saratani Kitaifa nchini Italia, kwa kushiriki kikamilifu katika taasisi na miundo mbinu ya huduma za afya inayomilikiwa na kuendeshwa na Serikali, taasisi pamoja na watu binafsi, ili kuzisaidia familia zilizoathirika kwa ugonjwa wa Saratani katika maisha yake ya kila siku!. Huu ni ushuhuda wa Kikanisa unaofumbatwa katika maisha na utume wa Kanisa ili kuonesha mshikamano wa dhati na watu wanaoteseka kwa kuwahudumia kwa unyenyekevu na katika hali ya ukimya pasi na majigambo wala makelele!

Baba Mtakatifu anakaza kusema, hii ni huduma makini inayojielekeza zaidi kwa watu wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii mintarafu: mahusiano ya kijamii, hasa pale magonjwa yanapoharibu utaratibu wa maisha ya kila siku na kwa namna ya pekee, ugonjwa wa Saratani. Hali hii inawaalika watu wote kuwajibika zaidi na zaidi, ili kuzima kiu ya ukweli na wema; mambo ambayo ni chombo cha neema ya Mungu. Kuwahudumia wagonjwa ni ushuhuda na utajiri mkubwa katika jamii, changamoto kwa waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kujenga utamaduni wa ujirani mwema; bila kuogopa kuwaonjesha wengine huruma na upendo; wala kupoteza muda unaojenga na kuimarisha faraja na mshikamano wa kweli!

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, afya bora ni sehemu ya haki msingi za binadamu, kumbe, mchakato wa kuzuia ugonjwa wa Saratani unapaswa kuelekezwa kwa watu wote, kwa njia ya ushirikiano kati ya taasisi za Serikali na zile za watu binafsi; umoja na mshikamano huu pia ujioneshe katika taasisi za kijamii na zile za huduma ya upendo. Hapa anasema Baba Mtakatifu, Jamii inapaswa kujikita katika utamaduni wa ujenzi wa mafungamano ya kijamii pasi na watu kutengwa. Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko amewashukuru na kuwatakia heri na baraka katika maisha na huduma yao kwa wagonjwa wa Saratani pamoja na kuwaweka chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria afya ya wagonjwa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.