2017-06-26 14:32:00

Vatican yafunguka kuhusu kutoweka kwa Askofu Shao


Dr. Greg Burke, Msemaji mkuu wa Vatican akijibu maswali ya waandishi wa habari waliotaka kufahamu kuhusu hatima ya maisha na utume wa Askofu Peter Shao Zhumin wa Jimbo Katoliki la Wenzhou, nchini China anasema, kimsingi Vatican inaendelea kufuatilia sakata hili kwa ukaribu sana ili hatimaye kufahamu kwa nini Askofu Peter Shao Zhumin ameondolewa Jimboni mwake kwa nguvu na kupelekwa mahali kusikojulikana kwa kipindi kirefu kwa sasa!

Familia ya Mungu Jimboni humo pamoja na ndugu, jamaa na marafiki zake, hadi sasa hawana taarifa ya mahali alipo Askofu Peter Shao Zhumin. Vatican inasikitishwa kwa tukio na matukio kama haya yanayokwamisha maridhiano kati ya watu na kwamba, Kanisa linatumaini kuwa Askofu ataweza kuachiliwa huru haraka iwezekanavyo na hatimaye, kurejea kati ya watu wake ili kuendeleza huduma kwa amani na  utulivu. Vatican inawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kusali kwa ajili ya kumwombea Askofu Peter Shao Zhumin pamoja na maisha na utume wa Kanisa Katolikinchini China.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.