2017-06-26 09:11:00

Papa Francisko: Iweni mashuhuda waaminifu kwa Kristo na Kanisa lake!


Kristo Yesu, baada ya kuwachagua na kuwatuma wafuasi wake kushiriki katika mchakato wa ushuhuda na utangazaji wa Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia, aliwaandaa pia kuweza kukabiliana kimasomaso na dhuluma pamoja na nyanyaso ambazo watakabiliana nazo katika maisha na utume wao! Lakini, anawahakikishia uwepo wake wa daima na kwamba, wao wana thamani kubwa sana machoni pa Baba yake wa mbinguni na kwamba, wasiwe na wasi wasi wala hofu kwa wale wanaoua mwili lakini hawana nguvu ya kuweza kuua roho! Yesu anapenda kuwahakikishia wafuasi wake kwamba, cha moto watakumbana nacho, watakataliwa na watu na hatimaye, wataweza hata kuuwawa! Hii ni hali inayotishia usalama wa maisha ya wafuasi wa Kristo, lakini ndio ukweli wenyewe!

Haya yamesemwa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Tafakari ya Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, Jumapili tarehe 25 Juni 2017. Wakristo wanapaswa kuyalinganisha maisha yao na yale ya Kristo Yesu aliyeteswa na watu waliofahamu maisha na utume wake; akakataliwa na wale aliowatendea miujiza na kuwashirikisha matendo makuu ya Mungu; akakanwa na kutengwa hata na wale waliokuwa watu wake wa karibu! Hatimaye, akafa kifo cha aibu Msalabani, huku akiwa amezungukwa na majambazi. Kutokana na ukweli huu, hakuna utume wala maisha ya Kikristo ambayo ni sawa na “maji kwa glasi” au “kuku kwa mrija”. Mateso, dhuluma na nyanyaso ni sehemu ya vinasaba vya maisha na utume wa Kikristo kama njia ya kuhakiki ukweli wa imani na mahusiano yao na Kristo Yesu.

Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini kuchukulia mateso na mahangaiko yote haya kama sehemu muhimu sana ya kuwa wamissionari, ili kukua na kukomaa katika kujiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu, Baba yao wa milele, ambaye kamwe hawezi kuwaacha watoto wake kumezwa na “mawimbi mazito ya bahari”. Katika kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu duniani, Wakristo watambue kwamba, hawako pweke pweke, bali Mwenyezi Mungu yuko pamoja nao na anawapigania. Ndiyo maana, Liturujia ya Neno la Mungu, Jumapili ya XII ya Kipindi cha Mwaka, katika Injili ya Yesu anakaza kusema, “Msiogope”.

Baba Mtakatifu anasikitika kusema, hata katika ulimwengu mamboleo, bado Wakristo wanaendelea kuteswa, kunyanyaswa na kuuwawa kikatili! Licha ya “patashika nguo kuchanika”, bado Wakristo wanaendelea kutangaza na kushuhudia kwa ujasiri, ari na moyo mkuu, imani yao kwa Kristo na Kanisa lake! Msimamo wao wa imani unawachangamotisha Wakristo wengine kufanya maamuzi magumu katika maisha na utume wao, kwa kuamua kuwa upande wa Yesu; kwa kushuhudia ujasiri wa imani kila siku ya maisha yao hata katika maeneo ambayo pengine yanaonekana kana kwamba, yana utulivu na amani duniani! Wakristo watambue na kukumbuka kwamba, wao wanatumwa kama kondoo kati ya mbwa mwitu, kumbe, mauaji, mateso na nyanyaso ni sehemu ya maisha na utume wa Wakristo. Kristo Yesu anawatuma ulimwenguni ili kuyachachua malimwengu kwa njia ya ukweli wa Injili ambao unakuwa ni nguzo ya ukweli wenyewe. Kwa njia hii anasema Baba Mtakatifu Francisko, daima Wakristo wataangaliwa kwa jicho la kengeza. Lakini pamoja na yote haya, kama alivyosema kwa wafuasi wake nyakati zile, hata leo hii anaendelea kusema “Msiogope”.

Hili ni neno ambalo Wakristo wanapaswa kulikumbuka wakati wote wanapokumbana na dhuluma, nyanyaso na mateso, badala ya kukata tamaa, wakaze uso kama gume gume na kusonga mbele katika kutangaza na kushuhudia imani, kwani Kristo Yesu yupo pamoja nao. Wasiwe na wasi wasi wala shaka, kwa wale wote wanaowapuuza na kuwakejeli, bali wasonge mbele ili kupambana katika kutangaza na kushuhudia Injili. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kuwaonya Wakristo wanaoishi kwa unafiki, kwa kujifanya wanatangaza Injili ya Kristo, lakini, wao ndio wapinga Injili wa kwanza. Kila mtu ni kito cha thamani mbele ya Kristo Yesu, kumbe, atawaongoza na kuwasimamia katika mapambano ya kushuhudia na kutangaza Habari Njema ya Wokovu.

Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko anawaalika Wakristo kujiaminisha kwa ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mama mnyenyekevu na jasiri aliyeambatana na Neno la Mungu katika maisha yake, ili aweze kuwasaidia kutambua kwamba, katika ushuhuda wa imani kinachopewa kipaumbele cha kwanza ni uaminifu kwa Kristo na Kanisa lake na kwamba, wamehesabiwa kuwa ni wafuasi wamissionari wa Kristo na wala si mafanikio yanayoweza kupatikana.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.