2017-06-24 16:42:00

Papa Francisko: Maji ni kito cha thamani kiheshimiwe!


Michezo ni sherehe inayofumbata furaha na tunu msingi za maisha ya binadamu ili kukuza na kudumisha mafungamano ya kijamii, dhidi ya mwelekeo wa sasa ambao unaionesha jamii kuwa kama kimiminika, kisichokuwa na msingi thabiti wala rejea kwa mambo msingi. Haya yamesemwa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi, tarehe 24 Juni 2017 alipokutana na kuzungumza na wanamichezo wanaoshiriki katika mashindano ya kuogelea yanayojulikana kama “Settecolli”.

Huu ni mchezo unaofanyika majini, lakini si kimiminika, kwani ni mchezo unaohitaji maandalizi thabiti, nguvu, ujuzi na uthabiti wa moyo! Baba Mtakatifu anawasifu kwa kuwa na uzoefu mkubwa sana katika maji, lakini amewakumbusha  kwamba, maji ni kito cha thamani kubwa, kinachopaswa kuheshimiwa, kulindwa na kutunzwa na wote kama alivyowahi kusema, wakati fulani Mtakatifu Francisko wa Assisi. Mchezo huu unaofanyika majini, uwasaidie kujenga na kudumisha utamaduni na mwelekeo mpya wa matumizi ya maji, kwani maji ni uhai na kwamba, pasi na maji, maisha ya binadamu yako hatarini!

Baba Mtakatifu anakaza kusema, Mwenyezi Mungu ni asili wa uhai wa binadamu na chanzo cha vyote vinavyoonekana na visivyoonekana kwenye uso wa dunia na kwamba, hata maisha ya Kikristo yanapata chimbuko lake katika alama ya maji, yaani Sakramenti ya Ubatizo. Maji wanayotumia wanamichezo hawa yanahitaji kuangaliwa kwa jicho la pekee; yanapaswa kuheshimiwa na wala si kuabudiwa; wanapaswa kutafakari ili kupata maana halisi ya kila wanacho tenda katika maisha; wawe na nguvu na ujasiri wa kushinda uchovu; huku wakipania kufikia lengo la mchezo wao.

Katika mashindano, wanamichezo anasema Baba Mtakatifu Francisko wanapaswa kuonesha na kushuhudia ukweli na uwazi katika michezo sanjari na unyofu wa moyo. Kwa kucheza ndani ya maji, wanamichezo wawe tayari kusimama kidete kupambana kufa na kupona na mambo yote yanayochafua maji na maisha ya binadamu! Baba Mtakatifu amewashukuru na kuwapongeza viongozi na wanamichezo kwa kumtembelea na mwishoni, amewapatia baraka zake za kitume, huku akiwataka kudumisha michezo katika ari, moyo na furaha ya kidugu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 








All the contents on this site are copyrighted ©.