2017-06-22 16:53:00

ROACO: Dumisheni Uekumene wa damu na huduma makini kwa watu!


Shirika la Misaada kwa Ajili ya Makanisa ya Mashariki, ROACO, limehitimisha mkutano wake wa tisini kwa kukutana na Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi, tarehe 22 Juni 2017. Tangu mwaka 1968, ROACO imekuwa ni chombo cha upendo na mshikamano kinachoratibiwa na Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki. Ni huduma inayotekelezwa kwa namna ya pekee kupitia pia Mabalozi wa Vatican katika nchi hizi bila kusahau mchango mkubwa unaotolewa na Shirika la Wafranciskani waliopewa dhamana ya kulinda maeneo matakatifu, ambao kwa sasa wanaadhimisha Jubilei ya Miaka 800 ya uwepo wao na huduma katika Nchi Takatifu.

Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake amelipongeza Baraza la Kipapa kwa Ajili ya Makanisa ya Mashariki kwa kuadhimisha Jubilei ya Miaka 100 tangu kuanzishwa kwake. Hii ni historia ambayo imepambwa kwa matukio  ambayo kwa kiasi kikubwa yalilitikisa Kanisa la Mashariki hasa kutokana dhuluma na nyanyaso Ulaya ya Mashariki na huko Mashariki ya Kati. Kumekuwepo na wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji kutoka Mashariki ya Kati hali inayodhohofisha ushuhuda na uwepo wa Wakristo huko Mashariki ya Kati, ingawa wamekuwepo huko kwa miaka mingi.

Baba Mtakatifu anapenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwani kuna baadhi ya nchi kwa sasa zimejikomboa kutoka katika tawala za kimabavu, lakini hali bado ni mbaya sana huko Siria, Iraq na Misri, ambako kuna watu wanateseka kutokana na vita ghasia pamoja na mashambulizi ya kigaidi. Matukio yote haya yamewaonesha waamini Fumbo la Msalaba wa Yesu, chemchemi ya mateso, lakini zaidi ni kisima cha wokovu! Kanisa kamwe haliwezi kutembea, kujengwa, kuungamana na kushuhudia pasi na uwepo wa Fumbo la Msalaba. 

Kutokana na changamoto hizi anasema Baba Mtakatifu kuna haja ya kukazia kwa namna ya pekee majiundo awali na endelevu ya Majandokasisi, ili waweze kuwa tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya uwepo na huduma kwa Jumuiya zao, lakini pia wanapaswa kutambua kwamba wanaweza kukutana na vishawishi vinavyotaka kuwatumbukiza katika mchakato wa kutafuta utambulisho wa kijamii, au uchu wa madaraka mintarafu mwelekeo wa kitamaduni na mazingira husika. Kutokana na changamoto zote hizi, Baraza la Kipapa na Wakala mbali mbali wa Misaada kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki hawana budi kujizatiti kuendeleza miradi inayokuza na kuliendeleza Kanisa, ili kweli Kanisa liweze kujisikia kuwa ni Kanisa.

Baba Mtakatifu anasema, hapa kuna haja ya kukuza na kudumisha ujirani wa kiinjili kati ya Wakleri ili waamini wao waweze kuonja faraja na upendo kutoka kwa Kristo na Kanisa lake. Hii ni changamoto ya kutunza ndani mwao neema ya kuendelea kujifunza kuwa wafuasi na kwamba, uongozi ni huduma. Mwelekeo huu wa maisha, utawasaidia Majandokasisi na Mapadre vijana kujitoa bila ya kujibakiza ili kushiriki katika kazi ya ukombozi iliyoanzishwa na Kristo Yesu, Msamaria mwema, anayethubutu kuinama ili kuganga na kutibu madonda ya historia ya binadamu kwa mafuta ya faraja na divai ya matumaini ya Kiinjili. Waamini wanapaswa kujisikia kuwa ni sehemu ya mawe hai ya ujenzi wa Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa na kwamba, Kristo mwenyewe ni Jiwe kuu la Msingi!

Makanisa ya Mashariki yanatunza kumbu kumbu hai ya : Makanisa, monasteri pamoja na maeneo walimoishi watakatifu, dhamana inayotekelezwa kwa msaada mkubwa wa ROACO, ili kuwawezesha waamini kuendelea kufanya hija katika maeneo yenye mizizi ya imani. Waamini wawe ni Mahekalu hai ya Roho Mtakatifu, lakini daima wakikumbuka kwamba, maisha yao yamehifadhiwa katika chombo cha udongo kilichouhishwa kwa nguvu ya Roho Mtakatifu, changamoto ya kudumisha majadiliano ya kiekumene yanayofumbatwa katika uekumene wa damu na huduma kwa wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta usalama, hifadhi na maisha bora zaidi. Huduma zinazotolewa na ROACO zinapaswa kuwa ni daraja kati ya Mashariki na Magharibi; kati ya nchi asilia pamoja na nchi zinazotoa hifadhi kwa wageni na wahamiaji. Mwishoni, Baba Mtakatifu amewaweka wajumbe wote hawa chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa Mungu na kwamba, anawahakikishia sala na sadaka yake katika maisha na utume wao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.