2017-06-22 17:39:00

Papa Francisko asema, kuna haja ya kujikita katika ujenzi wa amani


Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi, tarehe 22 Juni 2017 amekutana na kuzungumza na Mfalme Wille Alexander kutoka katika Nchi za Scandinavia aliyekuwa ameandamana na ujumbe wake pamoja na Malkia Màxima; ambao wamebahatika pia kukutana na kuzungumza na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican aliyekuwa ameambatana na Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa Mambo ya nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa mjini Vatican.

Baba Mtakatifu pamoja na mgeni wake, wamegusia tema mbali mbali zinazogusa mambo msingi ya kitaifa na kimataifa. Kwa mfano kuhusu umuhimu wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote; mapambano dhidi ya baa la umaskini duniani sanjari na mchango wa Kanisa katika mambo haya msingi waliyojadili kwa pamoja. Kwa namna ya pekee, wamegusia wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji; umuhimu wa watu kuishi kwa kuzingatia misingi ya haki, amani na maridhiano licha ya tofauti zao za kitamaduni na kwamba, kuna haja kwa familia ya Mungu kujikita zaidi na zaidi katika ujenzi wa amani na usalama duniani, hasa zaidi katika maeneo yaliyoathirika kwa vita. Mwishoni, wamegusia kuhusu Umoja wa Ulaya na changamoto zake kwa sasa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.