2017-06-21 12:57:00

Tamko la Viongozi wa dini, Serikali Zambia ni demokrasia au udikteta!


Nchi ya Zambia kwa sasa inakabiliana na changamoto kadhaa ikiwa ni pamoja na suala la utawala wa mabavu wa serikali ya Rais Edgar Chagwa Lungu, kukandamizwa kwa uhuru wa watu na uvunjwaji wa haki msingi za binadamu. Viongozi wa kidini nchini Zambia hivi karibuni wamefanya jitihada kupitia watumsihi wa Ikulu ili kuonana na Rais Lungu, kwa nia ya kufanya mazungumzano juu ya hali kitaifa nchini humo kwa sasa. Hata hivyo jitihada zao zimegonga mwamba, na sasa wameamua kwa pamoja kutoa tamko wakiwaalika waamini na wote wenye mapenzi mema kujichunguza dhamiri, kuutafuta ukweli na kushikamana ili kurudisha matumaini kwa wakazi nchini humo.

Tamko la viongozi wa dini nchini Zambia linaoongozwa na tafakari, ukweli utawaweka huru (Rej., Yohane 8:32), wakiwaalika wote kutenda mambo ya haki, kupenda kuwa na huruma na kuishi kwa unyenyekevu (Rej., Mika 6:8). Itakumbukwa kwamba tarehe 10 Aprili 2017, kiongozi wa upinzani Bwana Hakainde Hichilema alikamatwa kwa mashtaka ya makosa ya uhaini, kuwa anajaribu kumpindua Rais Lungu sababu hakupisha msafara wake barabarani. Jitihada za kidiplomasia zimekuwa zikifanyika ili kutatua suala hili lakini serikali ilisisitiza kusonga mbele na mashtaka mahakamani. Kati ya vikundi vilivyoingilia kati ni kutoka nchi za Marekani, Nigeria, Kenya, Zimbabwe, Afrika ya kusini, Umoja wa Ulaya.

Kitendo hiki kwa viongozi wa Kanisa ni kurudisha nyuma demokrasia ya nchi hiyo na kuendekeza uongozi wa kidikteta. Namna pia Bwana Hakainde Hichilema alivyokamatwa kwa kutumia kikosi kikubwa cha polisi na mbwa, ni matumizi ya vitisho ambavyo vinawakumbusha rai wakongwe, utawala wa kikoloni wa waingereza. Hakimu Greenwell Malumani alisema kwamba hapo Polisi hawakutumia maadili ya kazi yao, kwani pia aliteswa na kuwekwa katika mazingira yasiyo ya utu. Viongozi wa kidini wanahoji iwapo Zambia kweli ni nchi huru, au imebaki na fikra za ukoloni za kabla ya uhuru wao wa Oktoba 24, 1964.

Uongozi hasa wa kitaifa unahitaji kuwa uongozi katika kweli, uungwana, na uaminifu. Uongozi wa serikali ya Rais Lungu unaonekana kushindwa katika hili, wanasema viongozi wa dini nchini Zambia. Haiwezekani kupata upatanisho na uponyaji kwa njia za udanganyifu na mabavu, kwani uongozi wa sasa nchini humo, upo tayari kuvunja sheria ili tu kufanikisha manufaa ya walio madarakani. Hii ni hali ambapo ubaya unapingana na wema. Viongozi wa dini wanasisitiza kwamba wao wanasimama kupigania wema na haki, ambayo ni hija kwa kawaida inayohitaji viongozi jasiri na wafuasi hata kama ni wachache ili kuushinda ubaya.

Serikali ya Rais Lungu inaonekana kutumia vyombo vya dola kutishia watu na kuwatenda vibaya. Kwa namna hii, ingawa kuna vyombo vingi vya habari, lakini raia wa Zambia wanazibwa midomo kutoelezea maoni yao na kuikosoa serikali kwa uhuru. Mwendo huu unaonesha utawala wa mabavu, utawala wa kidikteta kwani ni utawala usiosikiliza watu, hakuna demokrasia.

Viongozi wa dini nchini Zambia wanasema, mtu hata kama ametenda kosa, sio uungwana wala utu kumtendea kinyama, kwani anabaki kuwa ni binadamu anayestahili kuheshimiwa utu wake. Hata huduma za kidini zinazotolewa katika magereza hazimaanishi kwamba viongozi wa dini wanatetea uharifu, hapana, bali ni tunu ambazo kila mmoja anaalikwa kuziishi katika kuwatendea wote kiutu. Hivyo wanamualika Rais Lungu kulitazama upya suala la Bwana Hakainde Hichilema na hali ya nchi kwa ujumla kwa sasa. Ni matumaini ya viongozi wa dini kwamba, yatafanyika mazungumzano yanayolenga kwenye upatanisho wa kweli ili kujenga taifa lenye amani na haki.

Na Padre Celestine Nyanda.

Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican.

 

 

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.