2017-06-21 16:35:00

Kanisa limempoteza kiongozi aliyekuwa na ari na moyo wa kimissionari


Baba Mtakatifu Francisko amesikitishwa sana na kifo cha Kardinali Ivan Dias, Mwenyekiti mstaafu wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu na Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Bombay, kilichotokea tarehe 19 Juni 2017 na kuzikwa, tarehe 21 Juni 2017. Katika salam zake za rambi rambi alizomwandikia Bwana Francis Dias, kaka yake Marehemu Kardinali Ivan Dias, Baba Mtakatifu anashukuru kwa wema na ukarimu alioushuhudia Kardinali Dias enzi ya uhai wake katika huduma za kichungaji.

Kwa namna ya pekee kabisa, Kardinali Dias alishiriki kikamilifu katika upyaishaji wa maisha ya kiroho na kimwili ya wananchi wa Albania. Baba Mtakatifu anaendelea kusema kwamba, ni kiongozi aliyeonesha ari na mwamko mkubwa wakati wa utume wake kama Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu. Baba Mtakatifu anapenda kuchukua fursa hii, kuungana na familia ya Mungu Jimbo kuu la Bombay inayoomboleza kifo cha Kardinali Dias, aliyejitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma za kichungaji Jimboni humo; akawa na mwono mpana zaidi katika sera na mikakati ya shughuli za kichungaji. Kwa hakika atakumbukwa na wengi. Baba Mtakatifu anamwombea Marehemu Kardinali Ivan Dias, mwanga na raha ya milele ili aweze kupumzika kwa amani, huku akiwa na tumaini la ufufuko wa wafu na maisha ya uzima wa milele. Anapenda kuiweka roho ya Marehemu Kardinali Ivan Dias mikononi mwa huruma ya Mungu na hatimaye, anatoa baraka zake za kitume kwa wote walioguswa na msiba huu mzito!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.