2017-06-21 16:45:00

Huduma kwa wakimbizi ipanie kujenga huduma ya upendo na mshikamano!


Kongamano la Jimbo kuu la Roma kwa Mwaka 2017 linaongozwa na kauli mbiu “Majiundo makini kwa vijana wanaopevuka” limezinduliwa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu, 19 Juni 2017 kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Laterano. Baba Mtakatifu amekazia kwa namna ya pekee kuhusu: Familia Jijini Roma; Mshikamano na vijana; umuhimu wa vijana kutembea kwa pamoja; elimu makini na endelevu; vijana wanaopevuka na changamoto zao; majiundo ya maisha ya kiroho” yote haya yanapaswa kupembuliwa kwa kina na mapana mintarafu Waraka wa Kitume, “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya upendo ndani ya familia”!

Baba Mtakatifu Francisko alitumia nafasi hii kukutana na kusalimiana na wawakilishi wa wakimbizi pamoja na wahamiaji wanaohifadhiwa kwenye Parokia mbali mbali za Jimbo kuu la Roma. Hadi sasa kuna jumla ya Parokia 38, taasisi na Mashirika ya Kitawa yanayotoa hifadhi kwa watu 121. Baba Mtakatifu kwa nyakati mbali mbali amekazia umuhimu wa Kanisa kuwa ni chombo cha huruma na upendo wa Mungu kwa kuwapokea na kuwakirimia wakimbizi na wahamiaji wanaolazimika kuzikimbia nchi zao kutokana na: vita na ghasia; mipasuko ya kijamii na kisiasa; hali ngumu ya uchumi na umaskini; dhuluma, nyanyaso na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Tangu tarehe 6 Septemba 2015, Baba Mtakatifu alipotoa mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuwakirimia wakimbizi na wahamiaji, Shirika la Misaada la Kanisa Katoliki, Caritas Roma, limekuwa likiendesha kampeni ya kutoa hifadhi kwa wakimbizi na wahamiaji; kampeni inayoongozwa na kauli mbiu “Nilikuwa mgeni mkanipatia hifadhi: mkimbizi nyumbani kwangu”. Huu ni ukarimu unaosimikwa katika tunu msingi za maisha ya Kiinjili zinazopania kujenga na kuimarisha mtandao wa umoja, upendo na mshikamano, ili hatimaye, wakimbizi na wahamiaji hawa waweze kuingizwa na kuwa ni sehemu ya maisha ya familia ya Mungu nchini Italia.

Baba Mtakatifu Francisko amewapongeza waamini wote kwa moyo wa upendo na mshikamano unaovunjilia mbali tofauti kwa kukazia zaidi utu, heshima na haki msingi za binadamu. Huu ni ukarimu wa kidugu unaovuka mipaka ya kidini, kitamaduni na mahali anapotoka mtu! Wawakilishi wa wakimbizi na wahamiaji kwa upande wao, wanawashukuru waamini kwa moyo wa huruma na upendo wanaowaonjesha kila siku, kiasi kwamba, wanajisikia kuwa wako nyumbani.

Wanamshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa kuwafungulia mlango wa moyo wake uliosheheni huruma na upendo kwa maskini na sasa wameonja pia ukarimu wa Kanisa, kwani kwa njia ya huruma na upendo, waamini wanaweza kuingia katika maisha ya uzima wa milele. Baba Mtakatifu anaendelea kukazia majadiliano ya kidini na kiekumene yanayofumbatwa katika huduma ya ukarimu na upendo; kwa kuheshimiana na kuthaminiana wakati wa raha na shida! Kwa njia hii anasema Baba Mtakatifu watu wanaweza kukuza na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu! Dini inapaswa kuwa ni chombo cha upendo na ukarimu. Baba Mtakatifu anakiri kwamba, si rahisi kuweza kuwapokea na kuwakirimia wakimbizi, anawashukuru kwa huruma, wema, upendo, ukarimu na urafiki ambao wameujenga pamoja na wakimbizi na wahamiaji! Mwishoni, Baba Mtakatifu aliwapatia wote baraka zake za kitume!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.