2017-06-20 11:33:00

Papa Francisko abainisha mambo msingi katika malezi ya vijana!


Kongamano la Jimbo kuu la Roma kwa Mwaka 2017 linaongozwa na kauli mbiu “Majiundo makini kwa vijana wanaopevuka”. Tema hii ni matunda ya tafakari ya kina inayotaka kuimarisha furaha ya upendo ndani ya familia, ili kweli familia za Kikristo ziweze kuwa ni mashuhuda na vyombo vya Injili ya familia kwa kujikita katika tunu msingi za maisha ya Kikristo na kiutu!  Linapania kuimarisha dhamana na wajibu wa wazazi na walezi kwa watoto wao katika masuala ya maadili na utu wema.

Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake elekezi kwa wajumbe wa kongamano hili aliyoitoa, Jumatatu, tarehe 19 Juni 2017 amekazia: Familia Jijini Roma; Mshikamano; umuhimu wa vijana kutembea kwa pamoja; elimu endelevu; vijana wanaopevuka na changamoto zao; majiundo ya maisha ya kiroho” yote haya yanapaswa kuangaliwa mintarafu Waraka wa Kitume, Furaha ya upendo ndani ya familia! Baba Mtakatifu ameanza kwa kumshukuru na kumpongeza Kardinali Agostino Vallini, Makamu Askofu Mstaafu wa Jimbo kuu la Roma aliyemsindikiza katika utume wake tangu siku ile alipochaguliwa kuliongoza Kanisa. Ni kiongozi ambaye ametumia karama na mapaji yake kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya familia ya Mungu, Jimbo kuu la Roma na kwamba, ataendelea kutoa huduma yake ndani ya Kanisa kadiri ya dhamana na wajibu wake kwenye Mabaraza mbali mbali ya Kipapa, kama mjumbe.

Mosi, Baba Mtakatifu Francisko amewataka wajumbe wa Kongamano la Jimbo kuu la Roma kupembua kwa kina na mapana matatizo, changamoto na fursa zilizopo miongoni mwa vijana wanaopevuka katika Jiji kama la Roma. Waangalie kwa kina na mapana maisha ya familia, malezi na majiundo ya vijana katika masuala mtambuka. Changamoto ya kazi, umbali, gharama ya maisha na changamoto za mtindo wa maisha Jijini ni kati ya mambo ambayo yanagumisha wazazi na walezi kuweza kutekeleza vyema wajibu wao. Kutokana na sababu mbali mbali, watoto wengi wanajikuta sehemu kubwa ya maisha wakiwa peke yao, hali ambayo ni hatari kwa makuzi na malezi ya vijana. Yote haya yapembuliwe kwa tafakari ya kina na sala ili kuweza kuyaangalia yote haya katika uhalisia wa maisha na wala si mambo yanayoelea kwenye ombwe la maisha ya vijana wa kizazi kipya!

Pili, Baba Mtakatifu anasema, kuna haja ya kujenga mshikamano kati ya wanafamilia na hatimaye majirani katika ujumla wake. Kutokana na utamaduni mamboleo, kuna hatari kwamba, familia zinaanza kumeguka na kusambaratika kiasi hata cha kukosa utambulisho na mizizi inayowaunganisha kama jamaa moja! Hapa kuna haja ya kujenga mazingira yatakayowawezesha wanafamilia kujisikia kweli wako nyumbani na wanathaminiwa na kamwe familia isionekane kuwa kama gereza dogo! Vijana wapewe fursa ya kujifunza kwa juhudi, bidii na maarifa, lakini pia wapewe malezi yatakayowasaidia kuwajengea heshima, utu wema na uadilifu. Vijana wajengewe uwezo wa kujadiliana na wote katika ukweli na uwazi; wajifunze hekima na busara kutoka kwa wazee wanaoshirikishwa katika  maisha ya kifamilia badala ya kuwatenga kana kwamba, wamepitwa na wakati na hawana jambo ambalo wanaweza kuchangia katika malezi na makuzi ya vijana wa kizazi kipya!

Tatu, Baba Mtakatifu Francisko anazitaka Familia kuelimisha na kuwafunda vijana wa kizazi kipya, huku wakiandamana nao hatua kwa hatua, ili kuweza kukabiliana na changamoto zinazoendelea kuibuliwa katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia. Ujana ni kipindi cha udadisi wenye maswali msingi yanayohitaji majibu muafaka; ingawa wakati mwingine hawana utulivu wa kuweza kusikiliza ushauri wanaopewa! Hii ni sehemu ya maisha ya ujana. Vijana wanapopevuka wanaibua changamoto kubwa katika maisha, lakini hiki ni kipindi muhimu sana kwa wazazi kuwa karibu zaidi na watoto wao! Ni wakati wa majaribu na hatari za maisha, lakini zaidi ni wakati wa ukuaji wa vijana na familia katika ujumla wake; ni kipindi cha kujenga matumaini kwa leo na kesho iliyo bora zaidi. Wazazi na walezi wawe makini, wasiwabane sana watoto wao kiasi hata cha kuchukia maisha.

Ujana si ugonjwa unaopaswa kutafutiwa dawa ya mchunguti anakaza kusema Baba Mtakatifu Francisko. Wazazi na walezi wawasindikize watoto na vijana wao ili waweze kukua na kukomaa, ili hatimaye waweze kushiriki katika kuandaa ustawi na maisha yao kwa siku za usoni. Katika kipindi kama hiki, vijana wanatamani kuwa marubani wanaoongoza maisha yao. Ndugu, jamaa na marafiki wa familia wasaidie kukuza na kudumisha tunu bora za maisha ya vijana kwani kuna hatari wakati mwingine, watu wa karibu na familia wakasababisha majanga ya watoto na vijana katika maisha yao. Wazazi na walezi wawe ni mfano bora wa kuigwa, kwa kuonesha dira, mwongozo na ndoto ambazo vijana wao wanaweza kuzitekeleza katika maisha kwa kutambua pia kwamba, maisha si lele mama kuna changamoto zake; kuna kushuka na kupanda; kuna kusuka na kunyoa! Yote haya yataka moyo kweli kweli! Baba Mtakatifu anazialika Parokia kukuza na kudumisha utume wa vijana, ili kuwasaidia kufanya maamuzi magumu katika maisha yao. Vijana wajengewe uwezo wa kushirikisha karama, vipaji, matumaini hata yale yanayowasambua kutoka katika undani wa maisha yao!

Nne, Baba Mtakatifu anakazia umuhimu wa kuwa na majiundo ya kina na endelevu yanayogusa undani wa mtu mzima: kiroho na kimwili: Ni majiundo yanayogusa: akili yaani masuala ya elimu; moyo: mambo ya mahusiano na mikono jinsi ya kufikiri na kutenda. Haya ni mambo msingi yakayowawezesha vijana wa kizazi kipya kukua na kukomaa, tayari kujisadaka na kujitoa bila ya kujibakiza ili kuchangia ustawi, maendeleo na mafao ya wengi! Haya ni mambo msingi yatakayowawezesha vijana kukuza utu na heshima yao.

Tano, Baba Mtakatifu Francisko anawataka vijana kuthamini ujana wao unaojikita katika utu, heshima na nidhamu na wala si ujana wa malumbano na majigambo yasiokuwa na kichwa wala miguu! Hata leo hii kuna malumbano makali kati ya wazazi na watoto wao! Katika hali kama hii, vijana wengi wanajikuta wanachanganyikiwa kiasi hata cha kupoteza dira na mwelekeo wa maisha. Kuna baadhi ya wazazi na walezi, wanataka kubaki katika maisha ya ujana kiasi kwamba, hawataki kuzeeka. Hizi ni dalili za watu kukosa maana sahihi ya maisha. Maisha ni safari inayofanyika hatua kwa hatua kutoka katika utoto, ujana hadi uzee, vinginevyo, jamii inaweza kujikuta ikiwa na wazazi ambao wamedumaa katika maisha.

Sita, Baba Mtakatifu anakazia umuhimu wa majiundo ya maisha ya kiroho, ili kujikita katika mambo msingi ya maisha badala ya kumezwa na malimwengu na kutaka kukimbizana na mitindo ya maisha, ulimbwende na ulaji kupita kiasi, hali ambayo wakati mwingine inageuka kuwa ni ugonjwa. Vijana wajifunze kuwa na kiasi, kujinyima na kuratibu vionjo vyao. Wakuze kipaji cha ugunduzi kwa kujenga na kudumisha utamaduni wa mshikamano, umoja na mapendo pamoja na ujenzi wa madaraja ya watu kukutana. Vijana watambue umuhimu wa kutumia vyema fursa, nafasi na muda walionao kwani muda ni mali. Umefika wakati kwa familia kujikita katika mchakato wa ujenzi wa umoja na mshikamano; sanjari na kujifunza kuwa watu wenye furaha katika mwelekeo mpya. Wazazi na walezi wanapaswa kujikita katika mchakato wa malezi makini kwa watoto na vijana wao, daima wakiendelea kujiaminisha na kumtegemea Mwenyezi Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.