2017-06-19 14:05:00

Wanahabari iweni vyombo na mashuhuda wa Injili ya amani duniani!


Shirikisho la Wanahabari Wakatoliki Duniani, Signis kuanzia tarehe 19 hadi 22 Juni, linaadhimisha mkutano wake wa mwaka unaowashirikisha wataalam wa mawasiliano ya jamii kutoka sehemu mbali mbali za dunia, huko Quèbec, Canada. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe ulioandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin katibu mkuu wa Vatican kwa ajili ya wajumbe wa mkutano huu, anawataka wajumbe kuhakikisha kwamba, wanajifunga kibwebwe kutumia vyema maendeleo ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano pamoja na mitandao ya kijamii, ili kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa, hususan katika mchakato wa uinjilishaji mpya!

Baba Mtakatifu anapenda kutumia fursa hii kuwataka wajumbe, kusimama kidete kutangaza na kushuhudia Injili ya amani duniani. Ujumbe wa Baba Mtakatifu umetumwa kwa Monsinyo Dario Edoardo Viganò, Mwenyekiti wa Sekretarieti ya mawasiliano mjini Vatican. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, wajumbe hawa watasaidia mchakato wa kukuza na kudumisha Injili ya amani duniani, mahali ambapo bado kuna vita, ghasia na mipasuko ya kijamii inayosababisha majanga makubwa kwa watu na mali zao.

Kwa upande wake, Kardinali Gèrald Cyprien Lacroix, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Quebec, Canada, kwanza kabisa anapenda kuwakaribisha Jimboni mwake. Anatumaini kwamba maadhimisho ya mkutano mkuu wa SIGNIS, utawajengea uwezo wadau wa tasnia ya habari kutambua na kuthamini mchango wao, tayari kusimama kidete ili kutangaza na kushuhudia Injili ya matumaini kwa wote. Wawe kweli ni mashuhuda wa Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa, wanapotekeleza dhamana na wajibu wao katika hali furaha na matumaini.

Mkutano huu unaongozwa na kauli mbiu “Vyombo vya mawasiliano ya jamii na ujenzi wa utamaduni wa amani”. Viongozi wakuu wa Shirikisho hili wanapembua kwa kina na mapana mchango wa wadau wa mawasiliano ya jamii katika ujenzi wa amani duniani; dhamana na nafasi ya Mwenyezi Mungu katika maisha ya watu. Wajumbe pia wanayo nafasi ya kusikiliza kwa muhtasari mchakato wa mageuzi yanayotekelezwa kwenye vyombo vya habari vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Vatican kwa wakati huu.

Vijana na matumizi ya mitandao ya kijamii; muziki na matumaini miongoni mwa vijana wa kizazi kipya ni kati ya mambo ambayo yanajadiliwa kwenye mkutano huu. Lakini, ikumbukwe kwamba, wanahabari wanao mchango mkubwa katika kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini na kiekumene; kwa kutangaza na kushuhudia ukweli badala ya mtindo wa sasa wa kutaka kukimbizana na “habari zilizochakachuliwa” au “fake news”. Washiriki watapata nafasi ya kuangalia Sinema “The Silence” inayoonesha jinsi ambavyo Mapadre watatu wa Shirika la Wayesuit walivyonyanyaswa na kudhulumiwa kutokana na imani yao kwa Kristo na Kanisa lake kunako karne XVII. Hii ni Sinema ambayo imechezwa na Martin Scorcese, ambaye, tarehe 21 Juni 2017 atapewa “Tuzo ya Signis” kwa Mwaka 2017.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican 








All the contents on this site are copyrighted ©.