2017-06-19 12:05:00

Papa Francisko: Onesheni upendo na mshikamano na wakimbizi


Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya tafakari juu ya Sherehe ya Ekaristi Takatifu, Jumapili, tarehe 18 Juni 2017 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, aliwakumbusha waamini kwamba, Jumanne, tarehe 20 Juni 2017, Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha Siku ya Wakimbizi Duniani ambayo kwa mwaka 2017 inaongozwa na kauli mbiu “Pamoja na wakimbizi. Kuliko wakati mwingine wowote, hatuna budi kuwa upande wa wakimbizi”. Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, kipaumbele cha kwanza hakina budi kutolewa kwa watu wanaokimbia kutoka katika vita, ghasia, dhuluma na nyanyaso mbali mbali.

Hawa ni watu wanaopaswa kukumbukwa kwanza kabisa katika: sala na maombi, watu waliopoteza maisha  kwa kuzama na kufa maji baharini na kwamba, makaburi yao hayana alama ya kumbu kumbu! Ni wakati wa kuwaombea watu wanaoteseka katika jangwa na utupu na hatimaye, kunyauka na kufariki dunia kutokana na njaa, kiu na uchovu wa safari jangwani! Historia ya machungu na matumaini ya maisha yanayobubujika kutoka katika undani wao inaweza kuwa ni fursa ya kukutana kidugu na kuanza kufahamiana.

Baba Mtakatifu anakaza kwa kusema, kwa hakika kukutana na wakimbizi pamoja na wahamiaji ni fursa inayoweza kufukuzia mbali woga na wasi wasi usiokuwa na mvuto wala mashiko; siasa na sera tenge kuhusu wakimbizi na wahamiaji na hivyo inakuwa ni chachu ya ukuaji kiutu, kiasi hata cha kuchochea ari, mawazo ya kuwa wazi, tayari kuanza kujielekeza katika mchakato wa ujenzi wa madaraja ya watu kukutana na kusaidiana.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.