2017-06-19 11:38:00

Moto unaendelea kusababisha majanga makubwa nchini Ureno!


Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili tarehe 18 Juni 2017, Sherehe ya Ekaristi Takatifu, ametumia nafasi hii kuonesha uwepo wake wa karibu kwa familia ya Mungu nchini Ureno inayokabiliana na moto mkali ambao tayari umekwisha sababisha majanga makubwa kwa maisha ya watu na mali zao kuzunguka eneo la Pedrògào Grande, kiasi cha kilometa 150 kutoka Lisbon, Ureno. Taarifa zinaonesha kwamba, zaidi ya watu 62 wamekwisha kupoteza maisha Baba Mtakatifu amewaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema waliokuwepo kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kusali kwa kitambo katika hali ya ukimya. Serikali ya Ureno imetangaza siku tatu za maombolezo kuanzia, Jumatatu, tarehe 19 Juni 2017.

Kwa namna ya pekee kabisa, Baba Mtakatifu Francisko ametambua uwepo wa wajumbe kutoka Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati pamoja na Umoja wa Mataifa waliofika mjini Roma ili kushiriki katika mkutano ulioandaliwa na Jumuiya ya Mtakatifu Egidio ili kuanzisha tena mchakato wa majadiliano ya amani na maridhiano kati ya wananchi wa Afrika ya Kati. Baba Mtakatifu anasema, bado moyoni mwake kuna chapa ya kumbu kumbu ya kudumu ya hija yake ya kitume nchini humo kunako mwezi Novemba 2015. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, kwa msaada na neema ya Mwenyezi Mungu pamoja na utashi wa watu wenye mapenzi mema nchini humo, wataweza tena kuanza kujikita katika mchakato wa amani ambao ni muhimu sana kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi!

Baba Mtakatifu ametumia nafasi hii kuwajulisha waamini kwamba, Jumanne, tarehe 20 Juni 2017 atafanya hija ya binafsi huko Bozzolo na Barbiana, ili kutoa heshima yake kwa Padre Primo Mazzolari na Padre Lorenzo Milani, Mapadre ambao walikuwa ni mfano bora wa kuigwa hata katika ulimwengu mamboleo. Baba Mtakatifu anatanguliza shukrani zake za dhati kwa wale wote wanaomsindikiza kwa njia ya sala na sadaka zao, lakini zaidi kwa Mapadre watakaomsindikiza kwa sala katika hija hii ya ushuhuda.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.