2017-06-17 18:19:00

Fumbo la Ekaristi Takatifu: Zingatieni toba na wongofu wa ndani!


Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwaichi wa Jimbo kuu la Mwanza katika mahojiano maalum na Radio Vatican anasema, Ekaristi takatifu ni chanzo na kilele cha maisha ya Kanisa. Anawataka waamini kukimbilia kiti cha huruma ya Mungu ili kuganga mapungufu yao ya kibinadamu na kuondolewa dhambi zao, tayari kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, chemchemi ya utakatifu wa maisha!

Maungano ya dhambi, yanawawezesha waamini kugangwa magonjwa ya maisha ya kiroho, tayari kuendelea na safari ya kujitakatifuza! Waamini wawe na mwamko wa kupyaisha maisha yao ya kiroho kwa kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa kwa ibada na uchaji badala ya kufanya mambo kwa mazoea, ili kweli maadhimisho haya yaweze kugusa undani wa mtu: kiroho, kiakili na kidhamiri. Ili kufikia lengo hili, Mapadre ambao kimsingi ni vyombo vya huruma ya Mungu wanapaswa kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa kwa heshima, nidhamu pamoja na kufanya maandalizi ya kina. Kuwepo na katekesi makini na endelevu kuhusu: ukweli wa dhambi, madhara yake kwa mtu binafsi na jamii katika ujumla wake.

Mapadre watenge muda wa kutosha ili kuweza kuwahudumiwa watu wa Mungu kwa wakati unaofaa badala ya kuadhimisha Mafumbo haya kwa kujisikia tu! Waamini wajenge utamaduni wa kuthamini na kukimbilia daima kiti cha huruma ya Mungu ili kujipatanisha na Mungu, jirani pamoja na mazingira yao, ili kweli dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi. Mapadre waguswe na mahitaji ya watu wa Mungu: kiroho, na wawe tayari kutekeleza wajibu, dhamana na utashi wa Mungu katika maisha yao. Kimsingi, Mapadre wakazie umuhimu wa Sakramenti ya Upatanisho inayowawezesha waamini kushiriki vyema Fumbo la Ekaristi Takatifu. Waamini wajitahidi kujenga na kudumisha dhamiri nyofu, ili kutambua uwepo wa dhambi na madhara yake katika maisha ya watu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.