2017-06-16 16:31:00

Mapadre Jimbo Katoliki Ahiara, mmewakwaza waamini kwa mgomo usiofaa!


Hivi karibuni mjini Vatican, Baba Mtakatifu Francisko kapokea ujumbe kutoka Nigeria kwa ajili ya kutafuta muafaka wa mamlaka na uangalizi wa kondoo wa Familia ya Mungu jimboni Ahiara. Katika kikao hicho, pamoja na wengine, walikuwepo pia Kardinali John Onaiyekan, Askofu mkuu wa Abuja na Msimamizi wa kitume wa jimbo la Ahiara, Askofu mkuu I. A. Kaigama Rais wa Baraza la Maaskofu nchini Nigeria, Askofu P.E. Okpaleke wa Ahiara na Kardinali Fernando Filoni, Mwenyekiti wa Baraza la kipapa la Uinjilishaji wa Watu.

Baba Mtakatifu Francisko akionesha masikitiko yake kufuatia hali ya utata ya jimbo la Ahiara, kalifananisha na mjane, sio kwa kupoteza mume bali kwa kumgomea Bwana harusi kuingia katika nyumba yake halali. Zaidi sana kalinganisha hali hiyo na mfano wa wakulima wadhulumati wa shamba la mzabibu wanaopanga njama za kutoa uhai wa mtoto wa mwenye mali ili wao walirithi (Rej. Mathayo 21: 33-44). Baba Mtakatifu Francisko anasema, jimbo la Ahiara ni kama bibi harusi anayemgomea bwana harusi wake na hivyo kugeuka kuwa mgumba, na kushindwa kuzaa matunda. Jimbo la Ahiara linapatikana maeneo ya Mbaise, Metropolitan ya Owerri nchini Nigeria. Jimbo hili lilianzishwa mnamo Novemba 18, 1987 chini ya Askofu Victor Adibe Chikwe, aliyefariki tarehe 16 Septemba 2010. Mnamo mwaka 2012 Askofu Peter Okpaleke aliteuliwa kuwa Askofu wa jimbo hilo, lakini mapadri na waamini walei wakagoma kumpokea Askofu Okpaleke kwa sababu siyo wa kabila la Mbaise, na anatoka jimbo lingine.

Mnamo Julai 3, 2013 Kardinali John Onaiyekan aliteuliwa kuwa Msimamizi wa kitume wa jimbo la Ahiara, wakati Askofu Okpaleke kashindwa kuingia jimboni humo na kuanza utume, kufuatia vitisho vilivyokuwa vikitolewa dhidi yake. Juhudi za Kardinali Onaiyekan kuwaelewesha wana Ahiara kumpokea Askofu wao hazikufua dafu. Mnamo tarehe 10 Januari 2015, Kardinali Peter Turkson, akiwa Mwenyekiti wa Baraza la kipapa la haki na amani, alimwakilisha Baba Mtakatifu jimboni Ahiara kutafuta suluhu ya suala hilo, bila mafanikio. Baba Mtakatifu Francisko anasema, baada ya jitihada zote zilizofanyika mpaka sasa kuwaelewa na kuwaelewesha wana Ahiara, umefika wakati wa kupiga hatua kuepuka kuendelea kuwaumiza Familia ya Mungu na hatari ya kuliangamiza Kanisa. Hali ya namna hii siyo tena suala la ukabila, bali ni tishio la kuteka shamba la mzabibu, lililo mali ya Bwana, anasema Baba Mtakatifu Francisko.

Katika hotuba yake kwa ujumbe kutoka Nigeria, Baba Mtakatifu anasema, ametafakari sana wazo la kulifunga jimbo la Ahiara, lakini ameona kwamba Kanisa kama Mama, haliwezi kuruhusu watoto wengi kama wao wateseke. Hata hivyo kaonesha kuumizwa sana na mapadri wa jimbo hilo wanaorubuniwa kumkataa Askofu wao na kumuwekea zuio la kuingia jimboni kwake kulichunga kundi la Bwana. Anayeendekeza mgomo huo anatenda dhambi ya mauti, jambo ambalo haliwezi kuendelea kuvumiliwa. Kwa sababu hiyo, Baba Mtakatifu ameagiza mapadri wote wa jimbo la Ahiara, walioko ndani na nje ya jimbo kiutume au kimasomo, waandike barua ya kuomba msamaha na kuahidi utii kwa Baba Mtakatifu. Barua ziandikwe na kila mmoja, binafsi, akionesha utayari wa kumpokea Askofu anayetumwa na Baba Mtakatifu, na Askofu wa jimbo hilo Peter Okpaleke. Barua hiyo inapaswa itumwe kwa Baba Mtakatifu ndani ya siku 30 kuanzia tarehe 9 Juni, ndo kusema kufikia tarehe 9 Julai 2017. Padre ambaye hatafanya hivyo, atakuwa amesimamishwa upadre na kuondolewa huduma zote za kipadre.

Hatua hii imeonekana kuwa ni ngumu na kali, lakini inalazimu kufanya hivyo sababu tabia zilizooneshwa na mapadri wa jimbo la Ahiara zimeikwaza Familia ya Mungu. Kristo aliagiza: yeyote anayeleta makwazo hana budi kushughulikiwa sawa sawa, amesema Baba Mtakatifu Francisko. Kardinali Onaiyekan kamshukuru Baba Mtakatifu kwa hatua aliyochukua na kwa ukaribu wa kibaba aliouonesha muda wote wa matukio ya Ahiara. Kwa upande wake Kardinali Fernando Filoni kamuomba Baba Mtakatifu ambaye kakubali kwamba, baada ya kuhitimisha suala hilo na kumpokea Askofu wao, Jimbo la Ahiara wafanye hija pamoja na Askofu wao mjini Vatican na kukutana na Baba Mtakatifu.

Padre Celestine Nyanda

Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican








All the contents on this site are copyrighted ©.