2017-06-16 07:00:00

Ekaristi Takatifu iwasaidie kujimega na kujitosa kwa ajili ya jirani!


Leo tunaadhimisha sherehe ya Mwili na Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo, yaani Ekaristi Takatifu. Wakati wa karamu yake ya mwisho ya Pasaka hapa, kabla ya kuteswa kwake, Kristo alitwaa mkate akaubariki akaumega na kuwagawia wanafunzi wake waule kama Mwili wake na divai wainywe kama Damu yake. Mkate na divai, bidhaa za kawaida katika maisha ya kibinadamu, na kwa nanma ya pekee katika mazingira ya uyahudi hupokelewa kama bidhaa muhimu kwa chakula cha kila siku zinatakaswa na kuwa mwili na damu ya Kristo. Zinageuzwa kuwa zawadi kutoka mbinguni na chakula chetu cha kiroho. Ni mkate kutoka mbinguni wenye utamu wa kila namna na wenye kumpendeza kila mtu.

Ekaristi Takatifu ni nguvu yetu tuwapo safarini kuelekea nchi ya ahadi, yaani mbinguni kwa Baba. Kwa kula chakula hiki tunaunganika na Kristo mwenyewe na Yeye anakuwa sababu ya utendaji wetu wa kikristo. Ni zawadi ambayo inatukukumbusha kuweka utegemezi wetu za daima kwa Mungu. Waisraeli katika somo la kwanza wanakumbushwa jinsi walivyoipokea mana iliyotoka mbinguni. Neno la Mungu linasema: “Akakutweza, akakuacha uone njaa, akakulisha kwa mana, usiyoijua wewe wala baba zako hawakuijua; apate kukujulisha ya kuwa mwanadamu aishi kwa mkate tu, bali huishi kwa kila litokalo katika kinywa cha Bwana”.

Ekaristi Takatifu ni uthibitisho kwetu wa uwepo wa daima wa Mungu pamoja nasi kwa njia ya Yesu Kristo. Hapa tunadokezewa kuwa tunapojiweka mbali na Mungu, tunapoacha kuhisi uwepo wake katika chakula hiki kitakatifu tutaangukia katika dhiki kuu. Ni maelekezo kwetu ya kupokea na kuyatenda yote kadiri ya mipango ya Mungu. Pamoja na kwamba walikula mana jangwani hawakujua asili yake kwa sababu haikuwa sababu ya nguvu au maarifa ya kibinadamu bali ni Mungu mwenyewe aliwalisha.

Ni funzo tunalipata kwamba mwanadamu katika utendaji wake wote, katika matamanio yake yote, katika yote ya maisha yake anapasika kuambatana na Mungu. Mana ya jangwani iliwapatia nguvu Wayahudi na kuendelea na safari ya Jangwani kuelekea nchi ya ahadi. Kristo katika Ekaristi Takatifu ni mana mpya inayotupatia nguvu ya kusonga mbele katika safari ya kiroho kwani kwa kuishiriki Ekaristi Takatifu tunaungana naye kabisa na kutufanya sisi kuwa sehemu yake na kutenda kama yeye.

Ekaristi Takatifu sana hutufanya sisi kugeuza mienendo yetu na kumwelekea Mungu. Hii ni kwa sababu Yeye aliye ndani ya fumbo hilo Takatifu anageuka kuwa kanuni ya maisha yetu. Wayahudi ambao waliila mana na kuwapa nguvu ya kimwili na hivyo kusonga mbele na safari walikumbushwa wakiambiwa: “Basi hapo moyo wako usiinuke, ukamsahau Bwana Mungu wako, aliyekutoa katika nchi ya Misri katika nyumba ya utumwa”.

Hapa wanakumbushwa juu ya matendo yao ya baadaye, kwamba yatoe shukrani kwa Mungu kwa wingi wa fadhili zake. Sasa, ikiwa chakula hiki ambacho kiliwapatia nguvu ya mimwili tu kiliwaweka katika hali hiyo ya kujibu kwa matendo mema ni vipi itakuwa zaidi kwa Ekaristi Takatifu, ambacho ni chakula cha kiroho na ambacho ni ishara ya ukombozi wetu kutoka utumwa wa dhambi na kutufanya kuwa wana huru wa Mungu na hutuunganisha na Kristo na kutugeuza kutenda kama yeye? Shukrani yetu inapata msukumo zaidi kwani matendo yetu mema yanafaidika na Yeye tuliyeungana naye na anayetenda ndani yetu.

Ukweli juu ya Ekaristi Takatifu unafafanuliwa vizuri katika somo la Injili. Kwanza Kristo anajitambulisha kuwa yeye ni chakula chenye uzima. “Mimi ndimi chakula chenye uzima kilichoshuka kutoka mbinguni”. Kristo anajitaja kuwa ndiye chakula hicho na anatuonesha chanzo chake kuwa ni mbinguni. Fumbo la umwilisho linafafanuliwa zaidi, yaani Kristo aliitwaa asili yetu ya kibinadamu kwa ajili kutupatia uzima, uzima ambao ulipotezwa na dhambi. “Chakula nitakachotoa mimi ni mwili wangu kwa ajili ya uzima wa ulimwengu”. Hapa anaunganisha chakula hicho na mwili wake mtakatifu ambao utatolewa na kuteswa msalabani kwa ajili ya ukombozi wetu. “Ekaristi Takatifu ni “Ukumbusho wa mateso na ufufuko wa Bwana … yaifanya iwepo sadaka ile moja ya Kristo Mwokozi inayojumlisha matoleo ya Kanisa” (KKK 1330).

Zaidi anakifafanua chakula hiki kuwa ni chenye uzima. Ekaristi Takatifu inatajwa kama chakula chenye uzima. Ndiyo! Ni chakula kinachotuletea uzima wa kiroho. Hapa tunarejeshwa tena katika wazo la hapo mwanzo kwamba bila Mungu hatuwezi kusonga mbele. Ekaristi Takatifu inakuwa kwetu alama uthibitisho wa Mungu ndani ya roho zetu na hivyo kuzifanya kuwa hai wakati wote na hivyo kusukumwa na kutenda kadiri anavyotaka Mungu kuelekea ukamilifu. Mungu hakumuumba mwanadamu mkiwa bali anamsindikiza daima katika safari yake hapa duniani. Hii inauthibitisha upendo wake mkuu na kuisimika nafasi yake adhimu katika maisha yetu. Kwa ufupi, bila Mungu katika maisha mwanadamu anakuwa mfu. Ekaristi Takatifu ambayo ni Sakramenti ya Mwili na Damu ya Kristo ni uhakika wa uhai wa kimungu.

Pili Kristo anatueleza wazi kwamba ni kwa kuupokea Mwili wake mtakatifu na Damu yake takatifu ndipo tunaungana naye. “Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu anao uzima wa milele; nami nitamfufua siku ya mwisho”. Uwepo wake kwetu si wa kinadharia bali ni katika kuungana naye kiukweli. Ekaristi Takatifu haituletei matunda yake kwa kuishangilia tu na kuielezea kwa maneno matamu matamu bali ni katika kuungana na Kristo kwa kuishiriki vyema. Kwa hakika tunapaswa kuishiriki vyema kwa kuzitakasa roho zetu kwani Yeye tunayempokea ni Mtakatifu sana na kwa mantiki ndogo tu anapaswa kukutana na kilicho kitakatifu kwani waingereza wanasema “Birds of the same feathers fly together”. Ni changamoto kwa wale wenye vizuizi vya kuijongea karamu hii takatifu kuweka sawa hali zao na kuishiriki kwa kustahili.

Tatu, Kristo anathibitisha kuwa chakula hicho ni kutoka mbinguni kama mana waliyoila Waisraeli njiani lakini anatofautisha kwa matunda yake. “Hiki ni chakula kishukacho kutoka mbinguni, si kama mababa walivyokula wakafa; bali akilaye chakula hiki ataishi milele”. Hili ni dokezo muhimu kwa ukuu wa Ekaristi Takatifu. Pamoja na kwamba Ekaristi Takatifu ni matunda ya kazi ya upendo wa Mungu kwetu kama zilivyo kazi zake nyingine kwetu, Ekaristi Takatifu inatugeuza kuwa wana warithi wa Mungu na hivyo kuwa hai daima. Mana ya jangwani iliwapatia Waisraeli nguvu ya kimwili tu lakini Ekaristi Takatifu inatuletea uzima wa kiroho. Uhai wa kiroho unadumu daima hata kama miile yetu itaonekana kuchakaa. Hii ni kwa sababu Kristo yu hai daima na hivyo tuunganikapo naye kwa imani tunaendelea kuwa hai daima. Kristo mwenyewe anasema: “Yeye aniaminiye mimi ajapokufa atakuwa anaishi” (Yoh 11:25)

Mtakatifu Agustino anaitaja Sakramenti hii takatifu kama “ishara ya umoja na kifungo cha upendo”. Ni tunu ya kimbingu ambayo ni sababu ya umoja kati yetu wanadamu. Mtume Paulo anatueleza juu ya umoja ulio matunda ya kiekaristi. Anasema: “Kwa kuwa mkate ni mmoja, sisi tulio wengi tu mwili mmoja; kwa maana sisi sote twapokea sehemu ya ule mkate mmoja”. Ekaristi Takatifu ni jawabu kwa jamii ya kibinadamu iliyosawijika kwa utengano. Kristo tunayempokea ni mmoja na kwa mantiki hiyo anapotugeuza na kutupatia uhai wa kimungu anatupatia hadhi ya aina moja, yaani kuwa wana warithi wa Mungu. Hakuna anayekuwa na hadhi ya juu au tofauti na mwingine kwani sote tunakuwa ni “Christopher” yaani, ”Wabeba Kristo”. Jamii ya kibinadamu iliyogawanyika ni usaliti wa fumbo hili na changamoto kwetu kwa kutokudhihirisha kile tulichokipokea.

Huyu ni Yesu, ni Mwili na Damu yake Takatifu sana. Tuangaziwe na mausia ya Mwenyeheri Mama Maria Crocifissa Curcio aliyesema: “Upendo mnaoupokea katika Ekaristi muuenezi kwa watu wote”. Tuuthibitishe uhai wa kimungu tulioupokea na kwa tendo la kuandamana na Ekaristi Takatifu katika mitaa na njia ya jamii yetu iwe ni ishara ya utayari wetu wa kuiishi Ekaristi Takatifu kwa kuyatimiza mapenzi ya Mungu.

Kutoka Studio za Radio Vatican ni mimi Padre Joseph Peter Mosha.








All the contents on this site are copyrighted ©.