2017-06-15 11:07:00

Lesotho: Uchaguzi umekwisha ni wakati wa upatanisho, umoja na amani!


Demokrasia ni mfumo unaowawezesha wananchi kushiriki kikamilifu katika maamuzi ya kisiasa, kwa njia ya chaguzi huru pamoja na kuwawajibisha viongozi wao kwa njia ya amani. Demokrasia ya kweli inafumbatwa katika serikali makini inayozingatia utawala wa sheria, utu na heshima ya binadamu; ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Baraza la Maaskofu Katoliki Lesotho pamoja na Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Kusini mwa Afrika, IMBISA, wamepongeza juhudi kubwa zilizofanywa na Tume ya Huru ya Uchaguzi, nchini Lesotho kwa kusimamia na kuendesha uchaguzi mkuu katika hali ya haki, ukweli na uwazi, kiasi kwamba, wananchi wengi wameridhia matokeo ya uchaguzi mkuu uliofanyika tarehe 3 Juni 2017.

Katika mchakato huu mzima, Kanisa lilituma waangalizi wa uchaguzi mkuu wapatao 120 waliotembelea na kukagua vituo vya kupigia kura 50! Waliangalia masuala muhimu kabla, wakati na baada ya kufunga zoezi zima la upigaji kura! Wasimamizi na maafisa wa uchaguzi mkuu walionesha weledi na kanuni maadili katika utekelezaji wa majukumu yao kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya nchi ya Lesotho. Walionesha ushirikiano na mshikamano na wapiga kura katika kutekeleza haki yao msingi kikatiba. Kimsingi walifahamu dhamana na wajibu wao kikamilifu. Wananchi walitimiza wajibu na vyombo vya ulinzi na usalama, vikasimamia ulinzi na usalama wa raia na mali zao!

Baraza la Maaskofu Katoliki Lesotho pamoja na Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Kusini mwa Afrika, IMBISA kwa wanasema, licha ya zoezi zima la uchaguzi kufanyika katika hali ya usalama na amani, kuna haja ya kuboresha zaidi masuala ya ulinzi na usalama, ili uwepo wa vyombo vya ulinzi na usalama visiwe ni tishio bali uhakika wa ulinzi na usalama wa wananchi na mali zao. Mazingira ya kupigia kura yanapaswa kuboreshwa zaidi kwa kutumia majengo ya serikali badala ya kutumia nyumba za watu binafsi na kwamba, watu wenye ulemavu wanapaswa kusaidiwa zaidi kwa siku za usoni.

Nembo ya Tume Huru ya Uchaguzi Lesotho ilipaswa kuonekana kwenye masanduku yote ya kupigia kura ili kuwajengea watu imani zaidi na hatimaye, kuondokana na tabia ya kulalama kila wakati baada ya uchaguzi kwa kisingizio cha kuibiwa kura! Maaskofu wa IMBISA wanasema, uchaguzi mkuu nchini Lesotho umehitimishwa na sasa kuna haja ya kuanza mchakato wa majadiliano na upatanisho katika ukweli, haki na amani miongoni mwa wanasiasa pamoja na wananchi, ili wote kwa pamoja waweze kushikamana katika mchakato wa ustawi, maendeleo na mafao ya wananchi wote wa Lesotho.

Serikali mpya ijitahidi kuganga na kuponya madonda ya utengani, chuki na uhasama miongoni mwa wananchi wakati wa mchakato wa uchaguzi mkuu. Vikosi vya ulinzi na usalama visaidie kulinda, kujenga na kudumisha haki, amani na usalama wa raia na mali zao! Viwango, weledi, ukweli, na uwajibikaji ni mambo msingi yanayopaswa kukuzwa na kuendelezwa zaidi na Tume Huru ya Uchaguzi nchini Lesotho. Siku ya kupiga kura si wakati wa kupiga tena kampeni, wananchi waachiwe uhuru wa kuchagua viongozi wao kwa kuongozwa na dhamiri nyofu! Kanuni ya dhahabu iwaongoze wananchi wa Lesotho katika kipindi hiki cha uongozi mpya.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.