2017-06-15 08:00:00

Jumuiya ya kimataifa kutoa kipaumbele kwa afya ya akili


Miaka 20 hivi iliyopita, Baraza la Kipapa la Wafanyakazi katika Sekta ya Afya lilifanya mkutano wa mwaka ili kutathimi kwa kina athari za kimwili, kihisia, kijamii na kiroho zitokanazo na afya ya akili. Aliyekuwa Baba Mtakatifu kipindi hicho, Yohane Paulo II alisema: yeyote aliyeathirika kwa afya ya akili, bado anabeba sura na mfano wa Mungu, kama vile binadamu wengine wote, na zaidi wanayo haki, siyo tu ya kuchukuliwa kama binadamu wenye sura na mfano wa Mungu, bali pia kuhudumiwa na kuheshimiwa hivyo. Askofu mkuu Ivan Jurkovic, Mwakilishi wa Kudumu wa Vatican kwenye Ofisi za Umoja wa Mataifa zilizoko mjini Geneva, Uswiss, katika kikao cha Baraza la Haki msingi za Binadamu, amekumbushia hilo, alipokuwa akichangia hoja juu ya wale wenye changamoto ya afya ya akili.

Ujumbe wa Vatican katika kikao hicho, umesifu sana uamuzi wa Baraza la Haki msingi za Binadamu la Umoja wa Mataifa, kuweka kipaumbele cha pekee kabisa kwa afya ya akili, kwani kwa miaka ya nyuma jambo hili lilikuwa linapotezewa sana, na pengine hata kuogopa kuligusia, kiasi cha kuwatenga wenye changamoto hiyo na kuishia kuwafungia kwenye wodi hospitalini au Nyumba zingine za matibabu ya afya ya akili.

Ni matumaini ya Vatican kwamba, mwaliko wa Jumuiya ya kimataifa kutowapotezea tena wenye changamoto za afya ya akili, itakuwa ni king’ora cha kuamsha dhamiri na hamasa kulitazama kwa undani zaidi suala hilo kwa kila anayehusika; kuanzia na watetezi wa haki msingi za binadamu, waundaji sera za afya, madaktari na wauguzi wa afya ya akili, wafanyakazi wengine katika sekta ya afya, wanafamilia, jamii mahalia, siku zote wakitambua thamani ya utu wa binadamu anayotunukiwa na Mungu Mwenyewe, na kwamba mwanadamu haipotezi tunu hiyo hata wakati ambapo afya yake kiakili inapoyumba.

Wahenga walisema: la mgambo likilia kuna jambo. Sasa limesikika la mgambo kutoka Baraza la Haki msingi za Binadamu la Umoja wa Mataifa, kutoa kipaumbele kwa afya ya akili, tujiulize kama kuna jambo, jambo hilo ni lipi! Tukiitazama jamii ya mwanadamu kwa muda mrefu sasa, mbali ya kuwafungia wenye changamoto ya afya ya akili, wamekuwa wakipewa dozi za dawa za usingizi na hivyo kuwafanya kuishi muda mwingi wakiuchapa usingizi. Watu hawa wamekuwa hawashirikishwi sana katika mwenendo wa matibabu yao, na hivyo kutokuwa na nafasi ya kujieleza, hivyo kuishia kupokea chochote kinachoamliwa na madaktari, wauguzi na wanafamilia. Mbaya zaidi, kwa baaadhi ya sehemu wamekuwa wahanga wakubwa wa kushawishiwa na kusaidiwa kujiua.

Kufuatia vita kama hizi dhidi ya utu wa binadamu, Baba Mtakatifu Francisko anasisitiza kwamba; maisha ya mwanadamu ni matakatifu, hivyo kila haki jamii inapaswa kwanza kabisa kuzingatia haki msingi ya kuishi kwa kila binadamu. Haki hii ya kuishi haitanguliwi na hali wala mazingira ya aina yeyote, iwe kisiasa, kiuchumi, au kinadharia. Kwa bahati mbaya mwanadamu leo ametengeneza utamaduni wa kutupatupa vitu kila baada ya muda mfupi, utamaduni huu wa kubadilibadili nguo, simu, vyombo vya usafiri na kadhalika, umepelekea kujengeka kwa kishawishi cha kutupilia mbali utu au hata uhai wa binadamu bila woga (Rej. Evangelii gaudium).

Askofu mkuu Ivan Jurkovic, anaialika Jumuiya ya kimataifa, sambamba na huduma ya afya kimwili, kijamii, dawa madhubuti, huduma ya kiroho pia ipewe nafasi kwa watu hawa. Huduma hii ya kiroho isitazamwe kana kwamba ni uponyaji wa kiimani unaotupilia mbali matibabu ya kisayansi, bali ni huduma inayofumbatwa pamoja na huduma zingine za kimatibabu.

Na Padre Celestine Nyanda.

Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican.

 

 

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.