2017-06-14 14:16:00

Waamini msiishie utazamaji, jitoseni ulingoni kuchuchumilia utakatifu


Umefika wakati wa wongofu wa ndani, wongofu wa kugeuza mtazamo wa waamini wanapokuwa wanaadhimisha sherehe au kumbukumbu za watakatifu, kutoishia kwenye kuwatazama tu katika ubora wa maisha yao ya utakatifu, bali kujifunza kutoka kwao na kuuchuchumilia utakatifu. Huu ni mwaliko wa Kardinali Leonardo Sandri, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki, wakati wa mahubiri alipokuwa akiadhimisha Misa Takatifu kwa kumbukumbu ya Mtakatifu Antoni wa Padua, siku ya Jumanne, tarehe 13 Juni 2017, kwenye Kanisa la mtakatifu Francisko jimbo la Rieti, nchini Italia. Imekuwa kawaida kwa waamini wakati wa kumbukumbu za watakatifu, kupozi kama watazamaji wa mashindano fulani, ambapo wanamtazama na kumshangilia mtakatifu anayekumbukwa siku hiyo, akipambana kuelekea taji la ushindi, na waamini wanatarajia kufaidika na taji hilo kwa maombi kupitia mtakatifu huyo.

Kumbe ni wakati wa kubadili mtazamo, wakati wa waamini kujisikia kuvutwa kushiriki katika mashindano hayo katika maisha ya kila siku, na bila kutishwa wala kukatishwa tamaa na magumu yaliyopo katika mashindano hayo, bali kukaza uso kama gumegume na kusonga mbele kwa bidii ili kufikia Hatima ya mashindano hayo, ambayo ni Kristo mwenyewe. Katika hilo, waamini waishi maneno ya mtume Paolo: sijidai kwamba nimekwishafaulu au nimekwisha kuwa mkamilifu, la hasha, bali nakaza mwendo ili kulipata lile tuzo ambalo kwa ajili yake Kristo amekwisha kunipata mimi (Rej. Wafilipi 3:12).

Kwa mfano wa mtume Paolo, waamini wanaalikwa kuiishi kweli katika ukarimu. Mtakatifu Antoni wa Padua ndivyo alivyoishi maisha yake, akikua siku hadi siku katika kumfuasa Kristo. Hamu kubwa ya kumfahamu Kristo ilikuwa dira kwa mtakatifu Antoni wa Padua, na aliweza kuwaambukiza hamu hiyo wale wote aliokuwa akikutana nao. Mtakatifu Antoni wa Padua alikuwa rafiki mkubwa wa Familia ya wana wa Mungu, na wengi walipata faraja katika kusikiliza Neno la Mungu na kupkea Sakramenti kupitia kwake.

Kardinali Leonardo Sandri anawaalika waamini kujitathimini namna ambavyo wanaweza kuishi kila siku kwa kumwilisha Neno la Mungu maishani mwao. Kila mmoja katika shughuli za kila siku, katika malezi ya watoto na vijana, ujenzi wa familia za kikristo, kuzingatia mafao ya wengi, kujitoa kuwa makasisi au kukumbatia maisha ya wakfu.

Kwa mtakatifu Antoni wa Padua, ukweli ulichukua mwili na kukaa kati ya wanadamu, kwani ukweli ni Kristo Mwenyewe. Kwa mantiki hiyo, mtakatifu Antoni aliuachia utajiri na kujimwilisha katika umaskini, ili kujitajirisha katika ushuhuda wa ukarimu na wema. Ukweli katika ukarimu sio mafundisho ya nadharia, bali ni mtu katika nafsi ya Kristo Yesu. Hivyo waamini wakumbatiwe na kutembea Naye katika hija ya maisha yao kuelekea Yerusalemu mpya. Kwa namna hii waamini watakuwa na uwezo wa kuwajali na kuwahudumia wagonjwa, maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Ili kufanikiwa utekelezaji wa hayo, waamini hawana budi pia kumwomba Bwana awape uwezo wa kukemea sumu mbaya ya chuki, uhasama, na uovu wa aina zote, sumu inayoelekea kumtafuna vibaya sana mwanadamu katika jamii ya leo.

Kardinali Sandri kawaalika waamini waendelee kuwaombea wale wote walioathirika na tetemeko la ardhi maeneo ya Amatrice, ili wasipoteze matumaini ya kuishi katika hali nzuri katika jamii yao iliyoharibiwa vibaya. Pamoja nao walioathirika kwa janga hilo asilia, kawaalika kuungana na waamini wa Iraq na Siria, wanaoathirika kwa tetemeko lingine la unyanyasaji na ghasia zinazosababishwa na mioyo wa baadhi ya binadamu, mioyo iliyoua dhamiri safi na kujiundia dhamiri ya chuki isiyomcha Mungu wala kumjali binadamu mwenza.

Na Padre Celestine Nyanda.

Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican.

 

 

 

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.