2017-06-14 15:19:00

Upendo ni chemchemi ya matumaini ya Kikristo


Upendo ni fadhila inayomwezesha mwanadamu kumpenda Mungu kuliko vitu vyote, kwa ajili yake mwenyewe; na jirani kama mtu anavyojipenda mwenyewe na yote haya ni kwa ajili ya mapendo ya Mungu. Hakuna mtu anayeweza kuishi bila upendo. Mateso na mahangaiko ya watu wengi katika ulimwengu mamboleo ni athari za kukosekana kwa fadhila ya upendo katika maisha yao. Watu wanajitaabisha kuonesha nguvu na uzuri wao kama kivutio cha kutaka kupendwa, na kwamba, kinyume cha hapa baadhi ya watu wanajisikia kuwa sawa na samaki nje ya maji! Watu wengi wanataka kujionesha ili kuzima kiu ya utupu wa ndani katika maisha yao!

Jambo la msingi kwa waamini ni kukuza na kudumisha utamaduni wa kupenda kwa uhuru kamili pasi na shuruti, ili kuiwezesha dunia kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi, lakini kwa bahati mbaya, kutokana na ukosefu wa upendo, dunia imegeuka kuwa ni Jehanamu. Tabia ya ubinafsi inayojionesha katika medani mbali mbali za maisha ya mwanadamu ni dalili za upweke hasi na hali ya kukosa upendo wa dhati! Katika mahangaiko mbali mbali ya mwanadamu, wengi wanajikuta wakijiuliza, inakuaje kwamba, hakuna mtu anayewathamini na kuitwa kwa majina yao?

Pale ambapo kijana anayepevuka anapogundua kwamba, hapendi na wala hapendeki, hapo unakuwa ni mwanzo wa “patashika nguo kuchanika” kwani kijana anageuka kuwa ni mtu mwenye ghasia na mgomvi kupindikia! Mifumo mbali mbali ya chuki na uhasama unaojionesha katika jamii ni kwa sababu kuna watu hawakuthaminiwa wala kuonja upendo katika maisha yao! Hakuna mtoto au kijana anayezaliwa akiwa mgomvi na mkatili; hakuna kijana mbaya duniani, bali kuna vijana wasiokuwa na furaha katika maisha, kwani wamekosa fursa ya kutoa na kupokea upendo; ni watu waliokosa dira na mwelekeo sahihi wa maisha; ni watu waliokosa kuonja tabasamu la kukata na shoka, kiasi cha kuwarudishia waliolitoa kwa bashaha na furaha!

Kwa bahati mbaya, kuna watu wanaoishi katika hali ya majonzi na huzuni kubwa, tabasamu la kweli linaweza kuwaamshia “cheche za furaha” na hapo wakaanza kuona njia ya kutoka  katika hali yao ya huzuni! Hii ni sehemu ya Katekesi ya Baba Mtakatifu kuhusu matumaini ya Kikristo, aliyoitoa, Jumatano, tarehe 14 Juni 2017 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, mjini Vatican. Baba Mtakatifu anakaza kusema, Mwenyezi Mungu ndiye anayepiga hatua ya kwanza kumwendea binadamu ili kumwonjesha upendo wa dhati, upendo usiokuwa na mawaa kwani Mungu ni upendo ambao kwa asili unaenea na kusambaa; ni upendo unaojisadaka. Upendo wa Mungu haufungamanishwi na wongofu wa binadamu, lakini pale toba na wongofu vinapojitokeza, haya yanakuwa ni matunda ya upendo wa Mungu.

Mtakatifu Paulo anafafanua upendo wa Mungu kwa kusema kwamba, Mwenyezi Mungu ameonesha pendo lake mwenyewe kwa binadamu kwa kuwa Kristo alikufa kwa ajili ya binadamu aliyekuwa anaogelea katika dimbwi la dhambi. Kristo amekufa wakati binadamu akiwa bado katika dhambi, mbali na upendo wa Mungu kama ilivyokuwa kwa Mwana mpotevu. Mwenyezi Mungu kwa kumpenda mwanadamu, ameamua kutoka na kupiga hatua ya kwanza kumfuata, kwani anawapenda waja wake hata pale wanapotenda dhambi na kukengeuka. Huu ndio upendo unaooneshwa na wazazi hata pale watoto wao wanapokengeuka na kutopea katika malimwengu. Wazazi hawaombei haki jamii ifutwe, lakini daima wataendelea kuteseka kwani wanawapenda watoto wao hata kama ni wakosefu na wadhambi wa kutupwa!

Hivi ndivyo inavyojionesha hata mbele ya Mwenyezi Mungu, aliyemuumba mwanadamu kutoka katika utupu na kwamba, uhusiano uliopo kati ya Mwenyezi Mungu, Mwana na Roho Mtakatifu ni upendo; unaowaambata binadamu wote. Kwa njia ya Kristo Yesu, Mwenyezi Mungu amewanuia, akawapenda na kuwahitaji; akawapatia chapa ya sura na mfano wake usioweza kufutika mbele ya macho yake yenye huruma na mapendo! Mwanadamu ameumbwa ili kufurahia maisha yanayobubujikia uzima wa milele. Ili kuleta mabadiliko ya kweli kwa mtu mwenye moyo uliosheheni majonzi na simanzi, kuna haja ya kumkumbatia, ili kumwonesha kwamba, anaheshimiwa na kuthaminiwa na kwamba, jambo la msingi ni kuondokana na hofu na majonzi haya.

Upendo ni chemchemi ya upendo, unaobubujikia katika pendo kama ilivyo pia kwa chuki inayomtumbukiza mwanadamu katika kifo! Yesu aliteswa, akafa na kufufuka kwa wafu kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti na hatimaye, kumwonjesha huruma na msamaha kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Baba Mtakatifu Francisko anasema, huu ni muda wa ufufuko kwa wote; ni wakati muafaka wa kupangusa mavumbi ya kukata tamaa hasa wale ambao kwa muda wa siku tatu wamekaa kaburini! Upepo mwanana wa uhuru unapuliza na kuwaachia waamini chemchemi ya matumaini!

Ikumbukwe kwamba, Mwenyezi Mungu anawapenda watoto wake wote pasi na ubaguzi na kwamba, Mwezi Juni, Mama Kanisa anautolea kwa namna ya pekee kwa ajili ya Ibada kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu, kisima cha upendo na huruma ya Mungu kwa binadamu. Huu ni mwaliko kwa waamini kuwa waaminifu kwa upendo wa Mungu uliofunuliwa kwa njia ya Kristo Yesu, tayari kutoka katika ubinafsi wao na kuambata Ufalme wa Mungu unaowakirimia uhuru wa kweli! Roho Mtakatifu awawezeshe waamini kuwa ni vyombo na mashuhuda wa neema na baraka ya Mungu kwa walimwengu wote, kwa kuwashirikisha ile furaha ya kuwa ni wana wa Mungu. Mwishoni, Baba Mtakatifu amewapongeza Mapadre wapya kutoka Jimbo Katoliki la Brescia na kuwataka wawe wachungaji wema kadiri ya Moyo wa Mungu. Anawaalika waamini kuiga mfano bora wa Mtakatifu Antoni wa Padua, mhubiri mahiri na msimamizi wa maskini na wale wanaoteseka!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.