2017-06-14 16:03:00

Sheria ya Utoaji Mimba: Simameni kidete dhidi ya utamaduni wa kifo!


Uhai wa binadamu ni kitu kitakatifu sana kwa sababu tangu mwanzo wake unahusiana na tendo la Mungu la uumbaji na daima unabaki na uhusiano wa pekee na Muumba aliye peke yake hatima na kikomo chake. Mwenyezi Mungu ni asili ya uhai tangu mwanzo wake hadi mwisho wake. Kanisa linafundisha kwamba, hakuna mazingira au mamlaka yoyote yanayoweza kujitwalia haki ya kuharibu moja kwa moja kiumbe cha kibinadamu kisicho na hatia! Uhai wa binadamu sharti uheshimiwe na ulindwe kwa namna iliyo kamili tangu nukta ile ya kutungwa mimba, kwa kutambua haki ya uhai isiyovunjwa kamwe. Haki isiyoondolewa ya uhai wa kila binadamu asiye na hatia ni kitu cha msingi wa jamii ya kiserikali na utungaji wake wa sheria.

Baraza la Maaskofu Katoliki Uingereza na Wales, Jumapili, tarehe 18 Juni 2017 linaadhimisha Siku ya Uhai Kitaifa! Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa ajili ya maadhimisho haya anawaalika wale wote wanaomwamini Kristo Yesu kusimama kidete, kulinda, kutangaza na kushuhudia Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Baba Mtakatifu anawataka waamini kushirikiana na watu wote wenye mapenzi mema ili kujenga na kudumisha utamaduni wa uhai, ukweli na upendo. Ujumbe huu, umewasilishwa kwa Baraza la Maaskofu Katoliki Uingereza na Wales na Askofu mkuu Edward Adams, aliyeteuliwa hivi karibuni kuwa Balozi wa Vatican nchini Uingereza.

Askofu John Sherrington, Mratibu wa Maadhimisho ya Siku ya Uhai Kitaifa anafafanua kwamba, Baba Mtakatifu, anapenda kuiaminisha familia ya Mungu nchini Uingereza chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa walio hai, zawadi ya uhai wa watoto wake wote. Anawahakikishia sala, maombezi na sadaka yake kwa waandaaji na washiriki wote wa tukio hili, ambalo ni kumbu kumbu ya Miaka 50 tangu Sheria ya Kutoa Mimba ilipopitishwa nchini Uingereza, yaani kunako mwaka 1967.

Maadhimisho haya kitaifa kwa mwaka 2017 ni mwaliko kwa familia ya Mungu nchini Uingereza, Wales na Scotland kuwakumbuka watoto wote waliotolewa mimba, hata kabla ya kuuona uso wa dunia. Ni wakati muafaka wa kuwasaidia wanawake wajawazito wanaoelemewa na wasi wasi juu ya ujauzito wao! Ni wakati wa kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu ili kuomba huruma na upendo wake; tayari kujipatanisha na kuanza kutembea katika unyofu wa moyo! Maaskofu wanawaalika watu kutafakari kwa kina juu ya Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo, kwa kutambua na kuthamini zawadi ya maisha, tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake hadi pale mauti yanapomfika kadiri ya mpango wa Mungu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.