2017-06-13 07:48:00

Maaskofu Katoliki Panama: Siku ya Vijana Duniani 2019 & Walei


Baraza la Maaskofu Katoliki Panama hivi karibuni, limefanya hija ya kitume mjini Vatican, inayoadhimishwa walau mara moja kila baada ya miaka mitano, kwa kukutana na kuzungumza na Khalifa wa Mtakatifu Petro pamoja na waandamizi wake, ili kuangaia maisha na utume wa Kanisa mahalia, tayari kupokea ushauri, ili kuliwezesha Kanisa mahalia kusonga mbele kwa imani na matumaini. Maaskofu wa Panama walipokutana na Baba Mtakatifu Francisko waliweza kumpatia kwa ufupi maandalizi ya Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2019 huko Panama.

Maaskofu wa Panama, wamekazia pamoja na mambo mengine, umuhimu wa kukuza na kudumisha utume miongoni mwa vijana wa kizazi kipya pamoja na kuwashirikisha waamini walei katika maisha na utume wa Kanisa, tayari kushiriki katika mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto unaobubujika kutoka katika tunu msingi za maisha ya Kikristo na kiutu! Maaskofu wamejadiliana kwa kina na mapana, changamoto, matatizo na fursa zilizopo katika maisha na utume wa Kanisa kwa ndoa na familia nchini Panama.

Maaskofu wanasema, kwa sasa changamoto kubwa ni ajenda ya usawa wa kijinsia inayotaka kufuta tofauti kati ya mwanaume na mwanamke; kwa kukazia uhuru usiokuwa na mipaka; uhuru ambao unakwenda kinyume cha utashi wa Mungu katika maisha ya mwanadamu! Huu ni uhuru unaotaka kuhalalisha hata ndoa za watu wa jinsia moja, jambo ambalo ni hatari sana kwa kanuni maadili na utu wema; hizi ni dalili za watu kukengeuka na kutopea katika imani.

Baba Mtakatifu amekazia umuhimu wa waamini walei kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa, wakleri wawe na ujasiri wa kutoka kifua mbele ili kwenda pembezoni mwa maisha ya waamini wao, ili kuwajengea imani, matumaini na mapendo kwa Kristo na Kanisa lake! Waamini walei ni muhimu sana katika mchakato wa kuleta mageuzi katika medani mbali mbali za maisha ya familia ya Mungu nchini Panama! Lakini, ili waweze kutekeleza dhamana hii, hawana budi kujengewa uwezo zaidi kwa njia ya majiundo endelevu yanayofumbatwa katika: Biblia, Mafundisho Jamii ya Kanisa, Katekesi makini na ushuhuda unaofumbatwa katika tunu msingi za maisha Kikristo na kiutu!

Wakleri na watawa wasibaki Sakristia na Makanisani peke yake, bali wawe na ujasiri wa kushiriki katika medani mbali mbali za maisha ya waamini wao, ili kuwapatia dira na mwongozo sahihi wa kufuata, wao wenyewe wakiwa ni mashuhuda wa kile wanachoamini, wanahofundisha na kujitahidi kukiishi!  Mapadre na watawa wawe ni mashuhuda wa imani ya Kristo na Kanisa lake; imani inayomwilishwa katika matendo ya huruma na huduma makini kwa familia ya Mungu!

Baba Mtakatifu amewataka Maaskofu wa Panama kuimarisha utume miongoni mwa vijana wa kizazi kipya, kwani wao ni jeuri na matumaini ya Kanisa kwa leo na kesho iliyo bora zaidi! Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani yanapaswa kuangaliwa kuwa ni sehemu ya mchakato wa maisha na utume wa Kanisa miongoni mwa vijana wala si kama tukio kubwa linalokuja na kutoweka mara kama umande wa asubuhi!

Huu ni mchakato unaopaswa kuacha chapa ya kudumu katika akili, nyoyo na maisha ya vijana wa kizazi kipya, ili waweze kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa, tayari kuyatakatifuza malimwengu kwa karama ya maisha ya ujana wao sanjari na kipaji cha ubunifu! Vijana wengi huko Amerika ya Kusini, wanakabiliwa na changamoto ya: biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya; ukosefu wa fursa za ajira pamoja na mifumo mbali mbali ya utumwa mamboleo.  Kutokana na umaskini wa kipato, vijana wengi wanajikuta hawana fursa ya kuendelea mbele na masomo katika taasisi za elimu ya juu na vyuo vikuu. 

Yote haya yanachangia vijana kutaka kukimbia nchi zao ili kutafuta maisha bora zaidi nchini Marekani, lakini wakiwa njiani wanakumbana na “pazia la chuma”. Zote hizi ni changamoto katika maisha na utume wa Kanisa miongoni mwa vijana wa kizazi kipya. Lakini vijana wakiandaliwa vyema, wanakuwa kweli ni jeuri ya Kanisa na Jamii inayowazunguka! Vijana hawa wanapaswa kusindikizwa katika maisha na utume wao, ili waweze kufanya maamuzi magumu tayari kumtumikia Mungu katika wito na maisha ya kipadre, kitawa au ndoa.

Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa mwaka 2019 yataiwezesha Panama kuwa ni daraja linalowakutanisha vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia kusikiliza kile ambacho Kanisa linataka kuwapatia kama dira na mwongozo wa maisha! Ni fursa kwa vijana pia kujenga utamaduni wa majadiliano ya kiekumene katika sala na maisha ya kiroho; katika huduma na ushuhuda wenye mvuto na mashiko! Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2019 yanapania kuwa na mwelekeo wa kiekumene ili kujenga na kudumisha umoja katika utofauti uliopatanishwa kwa njia ya Damu Azizi ya Kristo! Licha ya tofauti mbali mbali zilizopo miongoni mwa Wakristo, lakini kuna mambo msingi yanayowaunganisha kwa pamoja: Imani yao kwa Kristo Yesu, Sakramenti ya Ubatizo na Maandiko Matakatifu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 








All the contents on this site are copyrighted ©.