2017-06-10 08:41:00

Papa Francisko anasema, kila mtu anayo nafasi yake katika ulimwengu!


Mfuko wa Kipapa wa Mtandao wa Shule Kimataifa “Schola Occurrentes” ulianzishwa na Baba Mtakatifu Francisko takribani miaka ishirini iliyopita huko Argentina. Leo hii mtandao huu umeenea katika nchi 190, ukiwa na shule zaidi ya 450, 000 zinazomilikiwa na kuendeshwa na Serikali, mashirika ya kidini pamoja na watu binafsi. Baba Mtakatifu Francisko kwa kutambua umuhimu wa elimu shirikishi kunako tarehe 13 Agosti 2013 akaupatia hadhi ya Kipapa na Kimataifa. Mtandao huu, umepata sasa ofisi zake mjini Vatican, ambazo zimezinduliwa na Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa, tarehe 9 Juni 2017.

Katika uzinduzi wa ofisi hizi, Baba Mtakatifu alipata salam na matashi mema kutoka sehemu mbali mbali za dunia kupitia kwenye tovuti mbali mbali. Amekumbusha kwamba, Mfuko wa Kipapa wa Mtandao wa Shule Kimataifa “Schola Occurrentes” unapania pamoja na mambo mengine: kukuza na kudumisha kipaji cha ubunifu; michezo kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa afya bora miongoni mwa watoto na vijana pamoja na kuwajengea wanafunzi umuhimu wa kupenda, kuthamini na kutumia vyema maendeleo ya teknolojia, ili kweli yaweze kuwa ni kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi!

Haya ni mambo msingi sana katika mchakato mzima wa kurithisha elimu miongoni mwa watoto na vijana wa kizazi kipya. Huu ni mfumo wa elimu ambao unawashirikisha watoto wote pasi na ubaguzi. Kila mtu ana utu na heshima yake, kumbe anapaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa na wote, kwani kila mtu anayo nafasi muhimu sana katika ustawi na maendeleo ya wengi. Watoto na vijana wengi zaidi anasema Baba Mtakatifu wanapaswa kupewa fursa ya kusoma ili kujiandaa vyema kuweza kutekeleza dhamana na wajibu wao ndani ya jamii kwa siku za usoni.

Baba Mtakatifu anaonya kwamba, utandawazi una faida na hasara zake; kwani licha ya mazuri yanayojitokeza huko, utandawazi unaweza kuwafanya watu kufutilia mbali tofauti zao msingi na kuwafanya wote kufanana. Utandawazi wa kweli wenye mvuto na mashiko anasema Baba Mtakatifu ni kuheshimu na kuthamini tofauti msingi za kijamii, ili kukua na kukomaa. Kila mtu anawajibika kutambua dhamana na wajibu wake katika maisha na jamii katika ujumla wake, ili kuweza kushiriki kikamilifu katika kuchangia ustawi na maendeleo ya wengi.

Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kuwashukuru wadau na taasisi mbali mbali za elimu wanaoendelea kuchangia kwa hali na mali katika uwepo wa Mfuko wa Kipapa wa Mtandao wa Shule Kimataifa “Schola Occurrentes”. Anaendelea kukazia umuhimu wa elimu inayofumbata na kuambata utajiri wa mtu mzima: kiroho na kimwili. Hizi ni tunu msingi zinazomwezesha mwanadamu kugundua utu na heshima yake inayojikita katika mapendo. Hapa kuna haja ya kukuza na kudumisha utulivu na kipaji cha ugunduzi. Sanaa, michezo, tamaduni na muziki ni njia mbazo zinamsaidia mwanadamu kupata elimu na majiundo makini yanayojenga madaraja ya watu kukutana, kushirikiana na kusaidiana pasi na kuwatenga wengine katika masuala ya kiuchumi, kisiasa na kitamaduni. Vijana wanakumbushwa kwamba, wao ni jeuri na matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi. Anawataka vijana kutumia vyema muda wa masomo ili kujifunza na kumwilisha tunu msingi za maisha ya kiroho na kimwili, ili kuweza kuwa na maisha bora zaidi kwa siku za usoni.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.