2017-06-10 13:53:00

Baba Mtakatifu Francisko, Viongozi wa kidini kwenye G7 Mazingira


Ni jambo la muhimu sana katika uhamasishaji wa utunzaji na matumizi mazuri ya viumbe duniani, kila mmoja kuwa na uwajibikaji wa pamoja. Mwaliko wa kupyaisha juhudi za kutambua na kutunza uumbaji, ambao ni zawadi ya Mungu kwa mwanadamu, ili dunia iwe mahali pazuri pa kuishi. Huu ni ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko, uliotiwa saini na Kardinali Petro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, kwenda kwa Askofu mkuu Matteo Zuppi, wa Jimbo kuu la Bologna, kufuatia mkutano wa majadiliano ya kidini kuhusu utunzaji wa uumbaji ulioandaliwa na Earth Day Italia, wakati wa mkutano wa G7 kuhusu mazingira.

Majira ya asubuhi, siku ya Ijumaa, tarehe 9 Juni 2017, wamekutana viongozi wa dini mbali mbali huko Bologna Italia, ili kuongeza chachu kwenye majadiliano juu ya mabadiliko ya tabia nchi, saa chache kabla ya kuanza kikao cha G7 kuhusu mazingira. Viongozi hao wa dini wametia mkwaju mwongozo wa tunu msingi za utendaji, mwongozo ambao utakabidhiwa kwenye mikono ya mawaziri wa G7 Mazingira, tarehe 11 Juni, ukisomwa na Askofu mkuu Matteo Zuppi wa Jimbo kuu la Bologna.

Lengo la kukutana viongozi hao wa dini na kutoa pendekezo la mwongozo huo ni kutafuta mshikamano wa kina zaidi na viongozi wa serikali katika kukabili changamoto ya mabadiliko ya tabia nchi. Mwongozo wa tunu msingi za utendaji, ni sehemu ya kukumbusha kwamba taasisi za kidini zina nafasi kubwa sana katika kuhamasisha raia duniani kubadili mwenendo wa maisha ili kuilinda sayari dunia na vyote vilivyomo, hasa mahali ambapo serikali mahalia zinaonekana kushindwa kufanya hivyo.

Mwongozo huo umeweka wazi nia ya kuhakikisha kwamba makubaliano ya Paris yanatiliwa maanani na kutekelezwa katika utunzaji wa uumbaji. Viongozi wa dini katika mwongozo wa tunu msingi za utendaji katika utunzaji wa mazingira, wamealika uwajibikaji wa nchi tajiri zaidi kuheshimu wanyonge na hivyo kuhakikisha sera zao za Nishati zinakuwa wazi na zinazokubalika, kwani hata changamoto ya wahamiaji baadhi ya sehemu inasababishwa na mabadiliko ya tabia nchi.

Baba Mtakatifu Francisko amewaahidi viongozi hao wa kidini kwamba anawasindikiza kwa sala zake za kibaba na baraka za kitume. Utayari wa taasisi za kidini kushirikiana kwa karibu zaidi na kwa mshikamano wa kina na serikali ni ishara nzuri sana yenye matumaini makubwa ya mafanikio katika kukabiliana na changamoto ya mabadiliko ya tabia nchi.

Na Padre Celestine Nyanda

Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.