2017-06-09 15:11:00

Papa Francisko: wanawake na wanaume washirikiane kujenga udugu!


Majadiliano ni mchakato unaopaswa kutekelezwa kwa njia ya ushirikiano makini kati ya wanawake na wanaume kwa kukazia kwanza: dhamana na wajibu wa wanawake; majiundo makini ya udugu kwa kujenga majadiliano yanayosimikwa katika maisha ili kuheshimiana na hatimaye kujenga urafiki katika jamii! Haya ni mambo makuu yaliyotiliwa mkazo na Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa, tarehe 9 Juni 2017 alipokutana na kuzungumza na wajumbe wa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya kidini waliokuwa wanafanya mkutano wao wa mwaka kuanzia tarehe 7 hadi 9 Juni 2017 kwa kuongozwa na kauli mbiu“Wanawake wanaelimisha udugu”.

Baba Mtakatifu anasema, dhamana na wajibu wa wanawake katika kuelimisha udugu ni muhimu sana katika mchakato wa udugu na amani; changamoto pevu katika ulimwengu mamboleo. Dhamana na wajibu wa wanawake kama waelimishaji wa udugu bado haijatambuliwa sana kutoka na matatizo na changamoto wanazokabiliana nazo wanawake; changamoto ambazo kimsingi zinagusa katika utu na dhamana yao. Wanawake na watoto ni waathirika wakuu wa machafuko, vita na kinzani za kijamii. Pale ambapo kuna chuki na uhasama waathirika wakuu ni familia na jamii husika kiasi cha kuwazuia wanawake kutekeleza dhamana na wajibu wao, hata kama wana nuia mamoja; vitendo vya wanaume wakati mwingine vinakwamisha juhhudi za wanawake kutekeleza dhamana yao ya kuelimisha udugu kwa ufasaha zaidi.

Baba Mtakatifu anakazia umuhimu wa kuwathamini na kuwaenzi wanawake katika jamii na ulimwengu mamboleo kwa kutambua uwezo wao wa kuelimisha udugu duniani, kwani wana uwezo mkubwa wa kurithisha karama na mapaji yao kwa jamii kwa kukazia umoja wa familia ya binadamu. Uwepo wa wanawake katika medani mbali mbali za maisha ya binadamu ni msaada mkubwa katika ngazi: mahalia, kitaifa na kimataifa bila kusahau nafasi yao katika maisha na utume wa Kanisa. Wanawake wana haki ya kutekeleza dhamana na wajibu wao katika medani mbali mbali za maisha ya binadamu; kwa kuhakikisha kwamba, haki zao zinalindwa na kudumishwa kisheria. Wanawake washirikishwe kikamilifu katika uhalisia wa maisha.

Baba Mtakatifu anawapongeza wanawake wanaoendelea kujitosa bila ya kujibakiza; huku wakiwa na utambuzi makini; wakati mwingine wakitekeleza yote haya kwa ujasiri na ushujaa mkubwa. Kuna wanawake ambao wametumia utajiri na sifa zao kama wanawake kuchangia katika ustawi na maendeleo ya wengi kama akina mama na walezi wa jamii. Baba Mtakatifu anawataka wanawake kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa elimu na malezi ya kidugu; kwa kuonesha ukarimu,kuheshimiana pamoja na kudumisha sifa njema ya umama. Nafasi ya wanawake katika sekta ya elimu ni ”sawa na uji kwa mgonjwa kamwe hawawezi kutenganishwa”.  Wanawake wana mchango na utajiri mkubwa katika malezi kama wanawake;  kwa uwepo wao, mahusiano yao na jinsi wanavyojiweka mbele ya maisha ya binadamu na maisha katika ujumla wake.

Kimsingi anasema Baba Mtakatifu Francisko, wanawake na wanaume wanapashwa kushirikiana kikamilifu katika elimu na majiundo ya udugu; amani kwa kushirikiana na kukamilishana. Kwa vile wanawake wanahusishwa moja kwa moja na Injili ya uhai wanaweza kusaidia zaidi kukuza na kudumisha moyo wa udugu; uhai na upendo, ili kuweza kujenga dunia itakayoweza kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi kwa wote. Kwa bahati mbaya, wanawake sehemu mbali mbali za dunia wameendelea kuwa mstari wa mbele kubeba dhamana na majukumu ya kifamilia na kijami wakati wa vita na mipasuko ya kijami pamoja na wakati wote wa kukabiliana na changamoto za maisha. Baba Mtakatifu anawapongeza wanawake kwa mchango wao katika kuelimisha udugu; kwa kuwashirikisha wote na kujenga mahusiano thabiti yanayovuka utamaduni wa kutojali wengine!

Baba Mtakatifu anaitaka jumuiya ya Kimataifa kujenga na kudumisha utamaduni wa kujadiliana kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa urafiki unaojikita katika misingi ya kuheshimiana na kuthaminiana; mambo msingi katika majadiliano ya kidini, ili kupambanua changamoto mamboleo zinazojitokea katika masuala ya kidini kwenye ulimwengu mamboleo unaojikita katika mwingiliano wa tamaduni mbali mbali. Wanawake wanaweza kushiriki kikamilifu katika uzoefu na mang’amuzi ya kidini hata katika ngazi ya kitaalimungu, kwani kuna baadhi yao wameandaliwa vyema hata katika uwanja wa majadiliano ya kidini: Wanawake wasitengwe na kudhani kwamba, mawazo ni kwa ajili ya wanawake peke yao tu!

Bali majadiliano ya kweli anasema Baba Mtakatifu Francisko, ni hija inayowashirikisha wanawake na wanaume; wanaopaswa kutembea kwa pamoja! Uwepo wa wanawake ni muhimu sana, kwani wao wanatabia inayoweza kusaidia mchakato wa majadiliano; kutokana na kipaji chao cha kusikiliza kwa makini; ukarimu na uwazi kwa wengine. Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko amewashukuru wajumbe wa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini kwa huduma makini wanayoitoa kwa ajili ya Kanisa la Kristo. Ni matumaini yake kwamba, wataendeleza mchakato wa majadiliano ya kidini na waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema wanaomtafuta Mwenyezi Mungu. Amewapatia wote baraza zake za kitume.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.