2017-06-09 14:01:00

Kanisa Ghana linaselebuka kurejeshewa shule zilizotaifishwa awali


Serikali ya Ghana inanuia kurudisha shule za Kanisa mikononi mwa wamiliki halali wa shule hizo ili waendelee kuziendesha. Nia hiyo imetangazwa rasmi hivi karibuni na Dr. Mathew Opoku Prempeh, Waziri wa elimu nchini Ghana, katika kikao cha wadau wa elimu nchini humo. Kanisa limepokea kwa furaha kubwa habari hizo, baada ya kuwa zimetaifishwa na kuendeshwa na serikali kwa miaka mingi sasa tangu nyakati za uhuru.

Askofu John Bonaventure Kwofie, Mwenyekiti wa kamati ya elimu Baraza la Maaskofu nchini Ghana anasema kwamba ingawa wajibu wa kuelimisha jamii ya Ghana ni wa serikali ya nchi hiyo, ni ukweli usiopingika pia kwamba serikali ya Ghana peke yake haina uwezo wa kutimiza vema wajibu huo. Kwa sababu hiyo ni muhimu kushirikisha wadau wengine wa elimu kama Kanisa.

Shule hizi zilitaifishwa na serikali kutoka kwa wamiliki sababu ya kutokuwepo sera nzuri za uendeshaji wa shule hizo. Nia ya serikali kuzirudisha shule hizo kwa wamiliki wake halali wa awali, ni ishara ya kutambua mchango mkubwa wa Kanisa katika sekta ya elimu na hasa lengo la awali la uanzishwaji wa shule hizo, anasema Askofu Kwofie. Hivyo uendeshaji wa shule hizo lazima siku zote uzingatie malengo hayo, vinginevyo mahusiano kati ya serikali na Kanisa yatayumba, na elimu itakosa mwelekeo. Dr. Prempeh, waziri wa elimu nchini Ghana, alitoa tangazo hilo katika kikao cha wadau wa elimu kilichokuwa na nia ya kuboresha elimu nchini humo. Hii ni ishara wazi kwamba serikali inatambua Kanisa kuwa ni chombo cha kuaminika katika kuboresha sekta ya elimu.

Baraza la wakristo nchini Ghana limepokea pia kwa furaha habari hizo, na tayari linaanza kuandaa namna ya kushirikiana na serikali katika kutengeneza mpango mkakati wa urudishwaji wa shule hizo kwa wamiliki. Wakati huo huo Bi Doris Ashun, katibu mtendaji wa elimu katoliki nchini Ghana anawaalika makatibu elimu majimboni kuhakikisha wanakuwa bega kwa bega na wadau wa elimu katika uongozi na uendeshaji wa shule za Kanisa kwenye maeneo yao, ili malengo ya uanzishwaji wa shule za Kanisa yaendelee kung’ara kama mshumaa uliopambwa kwa nta ya mama nyuki, nayo nyota ya asubuhi iukute bado ukiangaza.

Na Padre Celestine Nyanda

Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican.

 

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.