2017-06-08 13:51:00

Utunzaji safi wa mazingira ishara ya moyo safi


Suala la utunzaji wa mazingira ni wajibu wa wote. Wajibu wa kila jamii, wajibu wa wakulima, wafugaji, wavuvi, wazalishaji viwandani, wafanya biashara, waelimishaji, vijana, na wazee. Kila mmoja lazima ahakikishe anapambana kutunza mazingira, kwani ni wajibu mbele ya wanadamu wengine, wajibu mbele ya viumbe, na mbele ya Mungu. Mto safi unaashiria dunia safi, mazingira safi huashiria jamii safi, biashara safi huashiria moyo safi. Patriaki Bartholomeo wa kwanza, Askofu mkuu wa Constantinopoli amesema hayo wakati dunia imetoka kuadhimisha Siku ya Mazingira Duniani mnamo tarehe 5 Juni 2017.

Akitolea mfano wa uchafuzi wa mto Asopos nchini Ugiriki, Patriak Bartholomeo anasema inaonesha umuhimu wa uwajibikaji wa kila mmoja katika kutunza uumbaji. Serikali, taasisi mbali mbali, makanisa, watu wa dini mbali mbali, na raia wote duniani wajisikie deni hilo la kutunza aina zote za viumbe na mazingira, kwa kuzingatia matumizi mazuri na uwajibikaji katika yote. Hata hivyo changamoto zinazotokana na uchafuzi wa mto Asopos, ni fursa ya kufanya utafiti wa kisayansi wa namna ya kukabiliana na suala zima la mabadiliko ya tabia nchi, kwani tatizo la mazingira ni kubwa sana kwa sasa na linatishia usalama wa Familia ya binadamu.

Patriak Bartholomeo anasema, uharibifu wa mto Asopos, ni matokeo ya kutokuwa na miundo mbinu mizuri ya kulinda mazingira, hasa katika uzalishaji viwandani, na kukosekana kwa taratibu nzuri za kisheria zinazolinda mazingira. Pamoja na utafiti wa kisayansi unaofanyika ili kulinda mazingira, ni lazima kurudi kwenye mizizi ya tatizo lenyewe. Tatizo la uharibifu wa mazingira linasababishwa na kutokujali kwa mwanadamu, kutokuwa na mahusiano yenye uwiano mazuri kati ya mwandamu na mazingira asilia, na upungufu wa malighafi asilia kutokuweza kukidhi mahitaji ya mwanadamu leo. Biashara na utafutaji wa faida kubwa ndio umekuwa sababu kubwa ya uharibifu wa mazingira, ambapo katika yote utu wa mwandamu unaonekana kuzidi kupotezewa siku hadi siku. Askofu mkuu Bartholomeo tangu amechaguliwa kuwa Patriak wa kiekumene mnamo 1991, amejipambanua kwa kufuatilia kwa ukaribu sana suala la mabadiliko ya tabia nchi, na ukosefu wa usawa kijamii na kiuchumi.   

Na Padre Celestine Nyanda

Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican.

 

 

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.