2017-06-08 13:22:00

Itala Mela kutangazwa Mwenyeheri


Mama Kanisa tarehe 10 Juni 2017 atamtangaza Mtumishi wa Mungu Itala Mela kuwa Mwenye heri. Mwenyeheri Itala Mela aliishi kati ya mwaka 1904 na 1957. Alikuwa mwamini mlei aliyejiweka wakfu na kuishi kwa Waoblati Wabenediktini, akichagua jina la Maria wa Utatu Mtakatifu. Pamoja na kuwa afya yake haikuwa nzuri sana, alijituma sana kufundisha na kufanya shughuli mbali mbali za kitume. Baada ya mahangaiko makubwa ya kiafya, alifariki huko La Spezia, tarehe 29 Aprili 1957, akiwa na umri wa miaka 53.

Kardinali Angelo Amato, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la kuwatangaza Waamini kuwa Wenyeheri na Watakatifu, anamuelezea mama huyu kwamba aliliishi vema jina lake la maisha ya wakfu, Maria wa Utatu Mtakatifu, kwani Utatu Mtakatifu ndio ulikuwa kiini cha utume na maisha yake kwa ujumla. Maisha ya Itala Mela yanaweza kugawanywa katika hatua tatu kubwa. Hatua ya kwanza ni wakati wa ujana wake ambapo hakuwa na imani kwa Mungu, akiwa amerithishwa Ukani-Mungu na baba yake, hivyo alidharau sana mambo yote ya Kanisa na imani kwa Mungu.

Hatua ya pili ni pale anapojiunga na chuo kikukuu cha Genoa kwa masomo ya Fasihi, ambapo aliishi kwenye nyumba ya wanafunzi iliyokuwa ikisimamiwa na kuhudumiwa na masista wa Mama wa Utakaso. Mwaka 1922 alialikwa na masisita kushiriki katika sikukuu ya Mama Bikira Maria mkingiwa dhambi ya asili. Awali aligoma, lakini baadae akivutwa kwa upole na wema wa watawa hao, ikiwa ni pamoja na kujali kwao watu kwa heshima, moyo wao wa sala na uchaji kwa Mungu, alihudhuria Kanisa ambapo walikuwapo Mapadri Wakapuchini, akaungama. Kilikuwa ni kipindi cha mashaka na kukosa mwelekeo kiasi fulani kwa miezi kadhaa. Mungu alianza kuugusa moyo wake kwa namna ya pekee, na Itala Mela akasali akisema “Bwana, kama wewe upo, tafadhari jifunue kwangu”.

Hatua ya tatu ni pale ambapo binti huyu aliamua kurudia ahadi na maisha ya uaminifu ya ubatizo aliokuwa ameupokea utotoni. Baada ya kuirudia imani yake, Itala Mela alibaki imara kama chuma cha pua na alishakamana sawa sawa na Utatu mtakatifu kama kupe kwenye ngozi. Kutoka hapo hakuteteleka tena, akavuka vipingamizi vyote vya kisaikolojia, kiafya na kiroho akiuchuchumilia utakatifu mpaka kifo.

Imani yake kwa Utatu Mtakatifu, ndiyo ulimvuta binti huyu akajiweka wakfu kwa Ufukara, Usafi wa moyo na Utii kwa askofu wake, na zaidi sana akaishi maishi ya kieremiti. Alitamani siku zote kujitoa kamili kwa Mungu, akiwa binti mtiifu kwa Mungu Baba, mwanafunzi mwaminifu wa Kristo na tabernakulo ya Roho Mtakatifu. Ukarimu wa Utatu Mtakatifu ulimfanya Itala Mela ajitoe kwa wahitaji kwa upendo, wema na upole, ingawa hakuwa tajiri.

Kardinali AngeloAmato anasema, maisha ya Itala Mela, ni mwaliko sio tu kwa mapadri na watawa, bali hasa kwa walei kuchuchumilia utakatifu. Kila mwamini akiishi kwa uaminifu ubatizo wake, ataweza kweli kuwa mhudumu wa uinjilishaji mpya na wa kina. Jamii ya leo inahitaji utakatifu katika Nyanja zote za elimu, afya, familia, sehemu za kazi, utandawazi, uchumi, michezo, siasa na kadhalika. Huu ni mwaliko wa waamini walei kuishi kikamilifu utakatifu ili kuigeuza hali ya utamaduni na maisha ya kiroho katika jamii. Jamii inahitaji walei watakatifu wanaoweza kuzaa matunda ya ushuhuda wa wema na ukarimu.

Na Padre Celestine Nyanda

Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.