2017-06-08 09:41:00

Achana na wito! Kutoka ufundi Seremala hadi kufundisha Chuo Kikuu!


Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa Siku ya 91 ya Kimissionari Duniani kwa mwaka 2017 anakaza kusema, vijana ni matumaini ya utume wa Kanisa. Kristo Yesu, ni kiini cha Habari Njema iliyotangazwa na kushuhudiwa naye katika maisha yake. Ni habari ambayo inaendelea kuleta mvuto na mashiko kwa vijana wengi wanaojisadaka kwa ujasiri bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa familia ya Mungu duniani. Hawa ni vijana wanaonesha ushuhuda wa upendo na mshikamano, wa huduma na majitoleo kwa ajili ya huduma makini, tayari kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu katika medani mbali mbali za maisha!

Kwa kutambua umuhimu wa vijana katika maisha na utume wa Kanisa, Baba Mtakatifu Francisko anasema, ameamua kuitisha Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ua vijana itakayoadhimishwa mwezi Oktoba, 2018 hapa mjini Vatican. Sinodi hii inaongozwa na kauli mbiu “Vijana, Imani na Mang’amuzi ya miito”. Katika mahojiano maalum na Radio Vatican, Padre Josephat Celestine Muhoza, SDS anasimulia historia fupi ya wito wake kutoka katika ufundi useremala hadi kufumua vitabu vya wanafalsafa mahiri duniani na leo hii ni Daktari wa Falfasa, ukitaka unaweza kumwita, Rev. Fr. DR. Josephat C. Muhoza, SDS. Kwa miaka kadhaa amefundisha Chuo Kikuu Kishiriki cha Jordan, Morogoro, Tanzania. Kwa sasa anaendeleza utume huo kwa kufundisha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Tanzania.

Padre Muhoza anakiri kwamba, haikuwa rahisi kuweza kutambua wito na karama ambazo Mwenyezi Mungu alikuwa amemkirimia katika maisha, lakini kwa njia ya wakuu wake wa Shirika, wakaweza kumsaidia kukuza Imani na hatimaye, kung’amua wito wake wa Kipadre ambao kwa sasa anautoa kama pia huduma ya malezi na makuzi kwa vijana wa kizazi kipya! Huu ni mwanzo tu, wa kurasa za maisha na utume wake, tutakazoendelea kukusimulia kupitia Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.