2017-06-07 16:14:00

Wanawake katika malezi ya amani na udugu duniani!


Dhamana ya wanawake katika malezi ya elimu na udugu ndiyo tema inayofanyiwa kazi na wajumbe wa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini, lililoanza mkutano wake wa mwaka, Jumatano tarehe 7 Juni na unatarajiwa kuhitimishwa tarehe 9 Juni 2017 kwa kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko. Kardinali Jean Lous Tauran pamoja na wajumbe wote kwa pamoja watakuwa na tafakari kuu nne ambazo zitatolewa na Nuria Calduch Benages anayechambua kuhusu “Wanawake wanaelimisha udugu”; Sr. Raffaella Petrini anazungumzia kuhusu karama za wanawake mintarafu Mafundisho Jamii ya Kanisa katika ujenzi wa udugu.

Kwa upande wake, Marie Derain anapembua kuhusu ujenzi wa amani kwa upande wa wanawake.  Mama Clare Amos, kutoka Baraza la Makanisa Ulimwenguni anachambua kuhusu dhamana na wajibu wa wanawake katika ujenzi wa udugu kadiri ya mwelekeo wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni! Wajumbe wanashirikishana mang’amuzi na mawazo yao kuhusiana na changamoto ya ujenzi wa amani na udugu duniani. Askofu Angel Ayuso Guixot atawashirikisha wajumbe kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni. Taarifa zaidi inasema kwamba, huu ni muda muafaka wa kutafakari hali halisi kuhusu majadiliano ya kidini kati ya dini mbali mbali dunia, mafanikio, matatizo, changamoto na fursa zilizopo! Ni wakati wa kuangalia dhamana, wajibu na nafasi ya Jumuiya ya Wakristo katika majadiliano ya kidini bila kusahau mchango wa wanawake katika kukuza na kudumisha amani na udugu kati ya watu wa Mataifa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.