2017-06-07 14:48:00

Changamoto mpya katika matumizi sahihi ya rasilimali za bahari


Inavyoonekana kwa siku za usoni, shughuli za binadamu baharini zitaongezeka sana, kutakuwa na usafirishaji mwingi kufuatia uhitaji mkubwa wa uvuvi, uchimbaji madini, mafuta, gas asilia, na uvumbuzi. Kutakuwa na utafiti endelevu utakaopanuka sana katika Nyanja za sayansi, biashara na matumizi ya rasilimali baharini. Teknolojia pia itakua, ambapo itatengeneza fursa na kuboresha matumizi yenye afya ya rasilimali hizo. Kardinali Peter Turkson, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Maendeleo Endelevu ya Binadamu, kwenye mkutano wa Umoja wa Mataifa wa kutunza na kuboresha matumizi ya rasilimali za maji, anaialika Jumuiya ya Kimataifa kuzitazama changamoto hizi na kujiandaa kuzikabili.

Kuna haja ya kuboresha ufahamu na uchunguzi kuhusu rasilimali na shughuli ndani ya maji, kuboresha mbinu za utunzaji, kubadili mipango mikakati inayoendana na utunzaji bora wa mazingira, ikiwa ni pamoja na kukabili zile hatari za kumwaga acid baharini, na kuzingatia hali zote za watu wanaoishi kwa kutegemea usalama wa chakula na maji kutoka baharini. Changamoto hii, itumike kuboresha sera, sheria, taratibu na mtazamo wa kufanya ustawi wa uchumi na jamii vinaendana na utunzaji mazingira.

Kardinali Turkson anasema, uzalishaji na matumizi ya rasilimali za baharini yahamasishwe katika jamii mahalia na katika dunia nzima, wakati huo taratibu za kitaifa na kimataifa zihakikishe zinakemea matumizi hatarishi ya bahari. Katika hayo yote ni muhimu kuzingatia wanaume na wanawake wanaoishi katika maeneo ya ufukwe au kufanya shughuli zao majini, sababu mazingira ya binadamu na mazingira asilia yanakua au kuharibika kwa pamoja.

Baba Mtakatifu Francisko katika Barua yake ya Kitume kuhusu Mazingira, Laudato sì, anasisitiza kuwatazama kwa namna ya pekee wavuvi wadogo wadogo wanaoathirika kwa kupungua kwa samaki majini, bila kuwepo mpango wa kuhakikisha uwepo endelevu wa rasilimali asilia majini, na pia uchafuzi wa maji jambo linalohatarisha afya za maskini wasio na uwezo wa kununua maji safi ya chupa, na ongezeko kubwa la wakazi maeneo ya ufukweni ambao hawana sehemu zingine za kwenda.Kardinali Turkson anaialika Jumuiya ya Kimataifa, kuzingatia taratibu zilizopo za kulinda, kutunza na kutumia rasilimali za maji kimataifa. Izingatiwe pia tofauti kati ya utunzaji na matumizi endelevu, ambapo Umoja wa Mataifa una nafasi kubwa ya kulishughulikia suala hilo.

Na Padre Celestine Nyanda

Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.