2017-06-06 13:59:00

Furaha ya ndoa na familia sio nadharia, ni uhalisia wa maisha.


Katika maisha ya ndoa na familia ni mahali ambapo panapatikana upendo na furaha ya maisha ya mwanadamu. Ni mapenzi ya Mwenyezi Mungu tangu kuumbwa ulimwengu kwamba mwanamke na mwanamume waishi katika ndoa na kujenga familia, ambamo ndani yake watashirikishana upendo na furaha kati ya wanafamilia wote, kisha kushirikisha upendo na furaha yao kwa jamii inayowazunguka. Kwa namna hii maisha ya mwanadamu na furaha yao inakamilika ndani ya Mungu, katika Utatu Mtakatifu. Baba Mtakatifu Fransisko anasisitiza sana upendo na furaha hiyo katika Wosia wake wa Kitume, Amoris laetitia, yaani Furaha ya Upendo ndani ya Familia. Kufuatia Wosia huo, Maaskofu nchini Ubelgiji wametoa Barua ya kichungaji wakiwaalika wenye kushiriki huduma za kichungaji katika nafasi zao mbali mbali kuwaelimisha waamini vizuri juu ya Furaha hii ya Upendo ndani ya Familia.

Kuna changamoto nyingi sana leo katika suala zima la maisha ya ndoa na familia, suala la kuwa wazazi na walezi bora wa watoto, furaha na udhaifu wa mwanadamu, uaminifu na upendo wa dhati kati ya wana familia wote. Kufunga ndoa kunaonekana kutopendelewa na wengi siku hizi, zaidi sana kufunga ndoa kanisani, na wengine hata kujaribu kwenda kinyume kabisa na mpango wa Mungu wa kufunga ndoa moja, kati ya mwanamke na mwanamume. Kumbe ni muhimu sana kuwaelimisha tena waamini na wote wenye mapenzi mema juu ya mpango wa Mungu na furaha zinazopatikana katika kuishi kiuaminifu mpango huo, ili ndoa iliyonuiwa na Mwenyezi Mungu tangu awali iweze kurudi kwenye fashion, katika ubora wake na kupewa thamani yake.

Ndoa ni Sakramenti, yaani ishara wazi ya upendo na uaminifu wa Mwenyezi Mungu mwenyewe, ambapo mwanadamu pia anaalikwa kuishi uaminifu na upendo huo. Kadiri ya mafundisho ya Mtume Paulo, ndoa pia ni ishara ya mahusiano ya upendo kati ya Kristo na Kanisa lake. Ni katika familia, wanadamu wanajifunza nini maana ya kuishi, na zaidi sana, wanajifunza namna ya kuishi kwa pamoja, katika umoja na upendo wa kidugu.

Maaskofu wa Ubelgiji wanasisitiza kwamba, huko kujifunza maisha na namna ya kuishi pamoja kidugu, ni moja ya sababu kubwa familia zinapata thamani na nafasi ya pekee katika jamii. Ni utume wa Kanisa na wanakanisa wote, kuvumbua tena hiyo thamani ya familia bora katika jamii, na sio ubora wa mali, bali ubora wa tunu na maadili. Ni utume wa wanakanisa wote kuwajali wana ndoa, kuwatia moyo, kuwahangaikia kwa upendo, na kwa hali na mali katika changamoto zao, ili wazidi kudumu katika upendo na uaminifu wao, na kumshuhudia Kristo hata inapowabidi kujitoa sadaka kubwa, kwani katika yote hayo, Kristo yupo kati yao siku zote.

Nyaraka za Kanisa sio manyoya ya kupeperushwa na upepo, bali ni nyenzo msingi za kuwasaidia waamini wote katika kuuchuchumilia utakatifu. Mababa wa Sinodi ya familia, ambayo kutoka kwayo, tumepewa Wosia wa kitume, Amoris laetitia, Furaha ya Upendo ndani ya Familia, walikuwa na lengo la msingi la kuboresha maisha ya ndoa na familia. Kwa sababu hiyo ni muhimu sana kuona namna ya kutumia nyenzo hii ili iweze kweli kuzaa matunda yaliyonuiwa na Mababa wa Sinodi ya Familia, kwa ajili ya Familia ya Mungu kwenye kona zote duniani.

Kadiri ya maaskofu wa Ubelgiji, kati ya mambo msingi ya kuzingatia ni pamoja na maandalizi mazuri ya wale wanaotaka kufunga ndoa, kuendelea kuwasindikiza kwa misaada mbali mbali ya kiroho na ushauri walio katika ndoa, kisha kuwapokea kwa heshima na kuwasaidia wale ambao ndoa zao zimepata misukosuko ya namna moja ama nyingine, na pengine kuleta vidonda na maumivu makali kwa wanafamilia husika. Katika barua yao ya kichungaji, maaskofu wa Ubelgiji wanasisitiza wana ndoa watambue na kuzingatia sana tena sana kwamba, ndoa ni wajibu unaohitaji juhudi na sadaka kubwa ili kuishi kwa upendo na uaminifu, juhudi na sadaka ambazo zinawahusu wana ndoa wote wawili.

Izingatiwe sana umuhimu wa kuwaandaa vema wana ndoa ili kutambua uzuri na faida zilizomo ndani ya maisha ya ndoa na familia, wazitambue pia changamoto zilizopo katika maisha hayo, ni umuhimu kuweka juhudi kubwa na kujitoa sadaka kuhakikisha upendo na uaminifu, vinavyokumbushwa na vifungo vya ishara za pete za ndoa, vinapewa kipaumbele ili vidumu kati yao siku zote za maisha yao.

Maaskofu wa Ubelgiji wanakumbusha wote wanaohusika na kuwaandaa wana ndoa, mbali ya kuzingatia maandalizi ya kufahamu namna ya kuishi ukristo katika jamii ya leo, maana ya ndoa na familia ya kikristo leo, na maandalizi ya maadhimisho ya liturjia ya ndoa, ni lazima kuongeza maelekezo na maandalizi mengine yatakayoweza kuwasaidia kuishi vema, kwa uaminifu, kwa furaha na kwa upendo wakimshuhudia Kristo kwenye kila changamoto za maisha yao. Katika yote hayo, waimbe na kuishi utenzi wa upendo kama anavyofundisha Mtume Paulo: Upendo huvumilia, hufadhili, upendo hauhusudu, upendo hautakabari, haujivuni, haukosi kuwa na adabu, hautafuti mambo yake, hauoni uchungu, hauhesabu mabaya, haufurahii udhalimu, bali hufurahi pamoja na kweli, huvumilia yote, huamini yote, hutumaini yote, hustahimili yote. (Rejea IWakorintho 13: 4 – 7)

Na Padre Celestine Nyanda

Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.