2017-06-05 15:29:00

Siku ya Mazingira Duniani kwa Mwaka 2017 imetiwa mchanga!


Kwa miaka mingi siku ya Mazingira duniani imekuwa ikiadhimishwa kwa Wadau katika nchi mbalimbali kuchukua hatua chanya zinazohusu utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Siku hii pia imekuwa ni sehemu ya kampeni ya utoaji elimu juu ya maswala yanayojitokeza kuhusiana na mazingira. Kauli mbiu katika maadhimisho ya mwaka huu 2017 inasema “Mahusiano Endelevu Kati ya Binadamu na Mazingira” ikihamasisha jamii kuwa na urafiki endelevu na mazingira asilia ambapo kila mtu anapaswa kutambua, kufurahi, kujivunia na kulinda uzuri wa mazingira asilia na kuhamasishana ili kuyatunza na kuyahifadhi.

Maadhimisho ya mwaka huu yameingia mchanga baada ya Rais Donald Trump wa Marekani kuamua kwamba, Serikali yake inajitoa katika utekelezaji wa Itifaki ya Paris juu ya utunzaji bora wa mazingira iliyopitishwa mjini Paris, Ufaransa kunako mwaka 2015. Athari za mabadiliko ya tabianchi zinahitaji uwajibikaji wa pamoja, ili kushiriki kikamilifu katika utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Huu ni wajibu wa kuhakikisha kwamba, Jumuiya ya Kimataifa inatumia kikamilifu maendeleo ya sayansi na teknolojia ili kudhibiti kikamilifu athari za mabadiliko ya tabianchi sanjari na kutumia nguvu kwa ajili ya mchakato mbadala wa maendeleo endelevu na bora zaidi, unaojikita katika tunu za kiutu na kijamii.

Lengo ni kuhakikisha kwamba, uchumi wa dunia unakuwa ni kwa ajili ya huduma kwa binadamu, ili hatimaye, kujenga msingi wa haki na amani, ili kulinda na kutunza mazingira, nyumba ya wote. Mambo yote haya msingi yametupwa “kapuni” na Rais Trump wa Marekani anaendelea kujitenga katika utekelezaji wa changamoto za Jumuiya ya Kimataifa. Askofu Marcelo Sanchez Sorondo, Mkuu wa Taasisi ya Kipapa ya Sayansi anasikitika kusema kwamba, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa ukuaji na ustawi wa uchumi wa Marekani ni kuhatarisha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi duniani yanayoendelea kuathirika kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi! Kumbe, kuna haja kwa Umoja wa Ulaya, Umoja wa Afrika, China na India kuendelea kushikamana kwa ajili ya utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote! Mwelekeo wa Marekani kujiondoa katika utekelezaji wa Itifaki ya Paris umeshutumiwa sana na Jumuiya ya Kimataifa, kwani ni hatari sana kwa mafungamano ya kijamii, kisiasa na kiuchumi.

Kwa upande wake, Kardinali Reinhard Marx, Rais wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Ulaya, COMECE anasikitika kusema, kwamba, maamuzi ya Rais Trump yanatia dosari sana imani kwa maamuzi yanayotolewa na Jumuiya ya Kimataifa.  Kimsingi, Jumuiya ya Kimataifa ilidhani kwamba, baada ya majadiliano makubwa kwenye mkutano wa G7 pamoja na kukutana na Baba Mtakatifu Francisko na kupewa zawadi maalum ya Waraka wa Kitume wa “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote”, Rais Trump angeweza kubadilisha msimamo wake kuhusu utekelezaji wa Itifaki ya Paris, lakini matumaini yote haya yamefifia kama ndoto ya mchana kwa Rais Trum kuendelea kushikiliza msimamo wake huo kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa Amerika! Maamuzi haya ni hatari sana kwa: ustawi, maendeleo na mafao ya wengi na kwamba, inasikitisha kuona kwamba, mustakabali wa maisha ya watu duniani unatiwa kampuni kwa maamuzi ya nchi moja tu duniani! Kardinali Reinhard Marx, Rais wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Ulaya, COMECE anaitaka Jumuiya ya Kimataifa kutokatisha tamaa, bali kuendelea kuungana na kushikakamana kwa ajili ya utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 








All the contents on this site are copyrighted ©.