2017-06-05 14:49:00

Kardinali Husar, mtu wa watu amepumzishwa kwa amani!


Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuungana tena na familia ya Mungu Jimbo  kuu la Kyiv-Halyč nchini Ukraine, kumwombea na kumsindikiza katika safari yake ya mwisho hapa duniani Marehemu Kardinali Lubomyr Husar aliyezikwa, Jumatatu, tarehe 5 Juni 2017. Anawashukuru na kuwapongeza wale wote waliobahatika kwenda kutoa heshima zao za mwisho kwa Marehemu Kardinali Husar, kielelezo makini cha uongozi wa kimaadili ulioshuhudiwa na Kardinali Husar katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni. Amekuwa ni Baba na kiongozi wa maisha ya kiroho, kwa watu wengi nchini humo!

Hii ni sehemu ya ujumbe ulioandikwa na Baba Mtakatifu Francisko kwenda kwa Askofu mkuu Sviatoslav Shevchuk wa Jimbo kuu la Kyiv-Halyč nchini Ukraine. Marehemu Kardinali Lubomyr Husar ni kiongozi aliyelazimika kuishi mafichoni kutokana na dhuluma na nyanyaso dhidi ya Wakristo huko Ukraine! Licha ya changamoto zote hizi, lakini bado aliendelea kuwa ni mtu mwenye furaha; akabahatika kuwa ni Baba na kiongozi mkuu wa Kanisa la Kikatoliki na Kigiriki nchini Ukraine. Katika hali ya uzee na ugonjwa akaendelea kubaki kati pamoja na watu wake na kuendelea kuwa ni rejea kama Mwalimu wa matumaini. Alikuwa na uwezo wa kuzungumza na kueleweka na wengi, kiasi hata cha kugusa undani wa maisha yao!

Marehemu Kardinali Husar alikuwa na hekima ya Injili; Mkate wa Neno la Mungu uliomegwa kwa ajili ya maskini, wagonjwa pamoja na wale wote waliokuwa wanatafuta utu na heshima yao kama binadamu! Alikuwa anakemea na kukanya kwa ari na moyo mkuu; akaeleza na kufafanua mambo kwa kina na mapana; akawa kweli ni faraja kwa waamini na wale wasioamini; akawa ni shuhuda wa tunu msingi za maisha ya Kikristo, matumaini na wazi mbele ya mpango wa Mungu kwa watu wa Ukraine kwa siku za usoni. Alibahatika kuwa na neno kwa kila mtu aliyemwendea kwa ushauri; akaonesha utu na upole! Alipenda kujadiliana na vijana wa kizazi kipya na wao wakatambua hazina kubwa iliyokuwa imefichika kwake, wakawa wanamkimbilia kwa wingi!

Baba Mtakatifu anasema, anasikia uchungu sana moyoni mwake, anapowaza jinsi ambavyo Ukraine nzima, inasali kwa ajili ya kumkumbuka na kumwombea Marehemu Kardinali Husar, ingawa kwa sasa anapumzika kwenye makao ya Baba wa milele! Familia ya Mungu nchini Ukraine, wanaomwona kuwa ni mfano na mwombezi wao huko mbinguni; ili aendelee kuliombea taifa lake linaloteseka kwa vita na ukosefu wa usalama, kwa kutambua kwa hakika kwamba, upendo wa Kristo kamwe hauwezi kudanganya. Baba Mtakatifu Francisko anahitimisha ujumbe wake kwa kusema, kwa hakika Marehemu Kardinali Husar ameonesha uwepo wenye nguvu na mashiko katika maisha ya kiroho, kijamii  na katika historia ya Ukraine, changamoto na mwaliko kwa familia ya Mungu nchini Ukraine kuendelea kuwa aminifu kwa kwa mafundisho yake sanjari na kujiachilia mikononi mwa Mwenyezi Mungu, anawasihi waendelea kuonja uwepo wake mwanana kati yao! Mwishoni, anawapatia wananchi wote wa Ukraine baraza zake za kitume.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.