2017-06-03 16:56:00

Papa: Oktoba, 2019 ni kipindi maalum cha kuhamasisha utume wa Kanisa!


Mashirika ya Kipapa ya Kazi za Kimissionari kamwe yasigeuzwe kuwa NGO za kukusanya na kugawa msaada kwa Makanisa hitaji zaidi duniani, kwa jina la Khalifa wa Mtakatifu Petro. Haya ni mashirika yanayopaswa kutekeleza dhamana na wajibu wake mintarafu mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Ili kufikia lengo hili kuna haja ya kuwa na wongofu wa ndani, kumbe, wakurugenzi wa Mashirika ya Kipapa ya Kimissionari waombe msaada wa maombezi ya Mtakatifu Karoli Lwanga na wenzake, mashahidi wa Uganda, ambao Kanisa linawakumbuka, tarehe 3 Juni 2017.

Hii ni changamoto ambayo imetolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi, tarehe 3 Juni 2017 alipokutana na kuzungumza na wajumbe wa Mkutano mkuu wa Mashirika ya Kipapa ya Kimissionari aliyekazia umuhimu wa kupyaisha ari na moyo wa shughuli za kichungaji kwa kuiga mifano ya watakatifu na mashuhuda wa imani. Anasema, ameridhia kutenga mwezi Oktoba, 2019 kuwa ni kipindi maalum cha kuhamasisha ari na moyo wa kimissionari kwa Kanisa zima, kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya miaka 100 tangu Papa Benedikto XV alipochapisha Waraka wa Kitume “Maximum illud” yaani kuhusu “Utume”.

Huu ni waraka unaofumbatwa kwa namna ya pekee kabisa katika maboresho ya shughuli za kitume, utakatifu wa maisha; muungano thabiti na Kristo Yesu, ili kuweza kushiriki kikamilifu katika kutangaza na kushuhudia Injili inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili kwa watu wote pasi na ubaguzi. Watu wa familia ya Mungu wanapaswa kujikita katika ari ya utume na utakatifu wa maisha; mambo msingi katika maisha na utume wa Kanisa kwa nyakati zote. Mtu anayehubiri anapaswa kuwa kweli ni mtu wa Mungu.

Ili kuweza kupyaisha utume, kuna haja ya kuongoka na kumwilisha utume wa Kanisa kama fursa makini na endelevu katika kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu; tayari kuwashirikisha wengine, furaha ya kukutana na Yesu katika hija ya maisha. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, huduma ya msaada inayotolewa na Mashirika ya Kipapa ya Kimissionari inafumbata Injili inayowashirikisha Wakristo wote, yaani: wakleri na waamini walei katika utume wa Kanisa unaopania kuwaonjesha watu wote huruma na upendo wa Mungu. Oktoba, utakuwa ni mwezi maalum wa kusali, kutafakari kuhusu utume kama msingi wa uinjilishaji, utasaidia kupyaisha imani ya Kanisa, ili katika moyo wake, Fumbo la Pasaka la Yesu Kristo, Mkombozi pekee wa ulimwengu; Bwana na Mchumba wa Kanisa liendelee kutenda kazi yake.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, maandalizi ya maadhimisho ya kipindi hiki maalum cha kutangaza na kushuhudia Injili kilisaidie Kanisa kuwa daima katika mchakato wa kujiinjilisha kwanza. Jumuiya za waamini ziwe ni jumuiya za matumaini yanayomwilishwa katika uhalisia wa maisha kwa kuwashirikisha wengine. Ziwe ni Jumuiya za upendo wa kidugu; zenye utamaduni wa kusikilizana daima sanjari na kuamini kuhusu matumaini yanayofumbatwa katika Amri mpya ya mapendo.

Familia ya Mungu duniani, kuna wakati inashawishiwa sana na malimwengu kumbe kuna haja kwao kusikiliza matendo makuu ya Mungu yakitangazwa tena mbele yao; kwamba, wamemwongokea Mungu na wanaalikwa kuungana naye tena kwani daima familia ya Mungu inapaswa kuinjilishwa, ili kujichotea nguvu ya ya kutangaza na kushuhidia Injili. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, Jubilei ya miaka 10 tangu kuchapishwa kwa Waraka wa Kitume “Maximum illud”, Mwezi Oktoba, 2019 kitakuwa ni kipindi cha sala na shuhuda za watakatifu na wafia dini.

Itakuwa ni nafasi ya kufanya tafakari ya Kibiblia na Kitaalimungu; katekesi makini pamoja na matendo ya ukarimu, yatakayolisaidia Kanisa kuinjilishwa tena, ili kupata ari na nguvu ya kushuhudia upendo ule wa kwanza kwa Kristo: aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, ili hatimaye, kuinjilisha kwa kujikita katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko! Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko amewatakia wajumbe wote heri na baraka za Siku kuu ya Pentekoste. Anawaweka chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Malkia wa Mitume na Mama wa Kanisa; na kwa maombezi ya watakatifu Petro na Paulo, Mitume pamoja na maombezi ya Mashahidi wa Uganda, ili waweze kuwaombea wote!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.