2017-06-03 17:50:00

Papa Francisko anahimiza mshikamano katika kukabiliana na majanga!


Baraza la Kipapa la Utamaduni kwa mara nyingine tena, Jumamosi, tarehe 3 Juni 2017, limeandaa Treni ya Watoto kutoka Italia ya Kati, eneo ambalo hivi karibuni liliathirika vibaya sana kutokana na tetemeko la ardhi lililosababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Watoto 400 waliosafirishwa kwa Treni Maalum ya Watoto wamekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican, kwa kuongozwa na kauli mbiu “Walinzi wa kazi za uumbaji”. Watoto hawa wamemwilisha ujumbe huu kwa kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko, aliyewaonjesha kwa mara nyingine tena furaha na matumaini yanayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake, ili kuondokana na woga pamoja na wasi wasi waliokumbana nao wakati tetemeko la ardhi lilipoyakumba maeneo yao, hapo tarehe 24 Agosti 2016. Watoto hawa wanamshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu kwa kuonesha upendo na ukaribu kwao wakati wa shida na mahangaiko yao.

Tetemeko la ardhi liliwasababishia hasara kubwa, lakini Baba Mtakatifu Francisko aliwatia shime na matumaini ya kusonga mbele. Watoto wamemwelezea Baba Mtakatifu Francisko mateso na mahangaiko yao; kwa shule, nyumba na makazi yao kubomoka; kwa baadhi yao kuwapoteza rafiki, ndugu, jamaa na wazazi. Haya ni majanga asilia wanasema watoto hawa kwamba, wamejifunza mengi kutoka kwenye Waraka wa Kichungaji wa “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote”. Jambo la msingi ni ujasiri wa kuanza tena upya, kwa kushikamana kwa hali na mali na kwamba, shule ina mchango wa pekee katika maisha ya watoto. Baba Mtakatifu anasema, majanga asilia yanasababisha majeraha makubwa katika maisha ya watu, lakini kwa wale wanaomtumainia Mwenyezi Mungu anawakirimia ujasiri, ari na moyo wa kuanza tena! Mwishoni, Baba Mtakatifu amewashukuru na kuwapongeza watoto hawa kwa kumtembelea mjini Vatican na kumtumbuiza kwa muziki mwanana kutoka Rio de Janeiro.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.