2017-06-03 17:25:00

Papa acheni unafiki kuhusu biashara ya silaha duniani! watu wanakufa!


Biashara ya silaha kimataifa haina budi kupigwa rufuku, kwani badala ya kusaidia mchakato wa kuharakisha maendeleo endelevu ya binadamu, imekuwa ni chanzo kikuu cha kinzani na vita; uvunjwaji wa haki msingi za binadamu, na hatimaye, umaskini. Huu ndio ukweli unaopaswa kufahamika kwa Jumuiya ya Kimataifa. Hata leo hii, dunia bado inaishi katika hofu ya vita, mashambulizi ya kigaidi na vita ya kinyuklia. Kuna Vita Kuu ya Tatu ya Dunia inayoendelea kupandikiza utamaduni wa kifo, sehemu mbali mbali za dunia.

Vita si suluhu ya kuweza kukabiliana na changamoto zinazojitokeza katika ulimwengu mamboleo. Kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kuwekeza zaidi katika elimu, afya, fursa za ajira kwa vijana; ustawi, maendeleo na mafao ya familia nyingi zaidi badala ya kugubikwa na ubinafsi unaoendelea kusababisha maafa makubwa kwa maisha ya watu kutokana na biashara ya silaha duniani inayowaneemesha watengenezaji na wafanyabiashara ya silaha, lakini waathirika wakuu ni wananchi wa kawaida!

Kwa mara nyingine tena, Baba Mtakatifu Francisko anapenda kutoa kilio chake cha kinabii kwa kusema, biashara ya silaha duniani inaendelea kusababisha majanga makubwa katika maisha ya binadamu. Kuna vita, vitendo vya kigaidi  na mipasuko ya kijamii ambayo kimsingi inasababishwa na biashara haramu ya silaha duniani. Baba Mtakatifu katika nia zake za jumla kwa Mwezi Juni, 2017 anasali kwa ajili ya kukomesha biashara ya silaha duniani. Nia za Sala za Baba Mtakatifu zinaenezwa na kusambazwa na Mtandao wa Utume wa Sala.

Baba Mtakatifu anasema, ni jambo la kushangaza watu kujadiliana kuhusu amani duniani, lakini kwa upande mwingine, watu wanachakarika usiku na mchana kwa ajili ya kufanya biashara ya silaha duniani. Inasikitisha kuona kwamba, kuna baadhi ya viongozi wanaojidai kutafuta suluhu ya amani duniani, lakini kwa kupandikiza utamaduni wa kifo unaofumbatwa katika biashara ya silaha duniani. Watu wengi wanapoteza maisha kutokana na biashara hii haramu. Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuungana naye kwa ajili ya kuwaombea viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa  ili kweli waweze kujizatiti kufanya maamuzi magumu ya kusitisha biashara haramu ya silaha duniani; inayoendelea kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao sehemu mbali mbali za dunia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.