2017-06-02 15:41:00

Watu wa Mungu wanapaswa kuongozwa kwa upendo na moyo wa unyenyekevu


Kristo Yesu baada ya kukamilisha utume wake hapa duniani, kabla ya kupaa kwenda zake mbinguni kwa Baba yake, alimkabidhi Mtakatifu Petro, mdhambi kuliko wadhambi wengine wote dhamana ya kuchunga familia ya Mungu kwa kujikita katika unyenyekevu, huruma na upendo, hata kama itakuwa bado inaogelea katika udhaifu na mapungufu yake ya kibinadamu. Hii ni sehemu ya mahojiano kati ya Yesu na Mtakatifu Petro kando ya bahari ya Tiberia, mahali ambapo kwa mara ya kwanza alisikia wito wa kuacha yote ili kuambatana na Kristo Yesu.

Wanazungumza katika hali ya amani na utulivu wa ndani; ni mazungumzo kati ya marafiki wawili wanaofahamiana sana katika karama na mapungufu yao. Ni majadiliano ya kina baada ya Fumbo la Ufufuko wa Kristo kutoka kwa wafu! Yesu Mfufuka anamdhaminisha Mtakatifu Petro kuwachunga kondoo wake kwa kumtwanga maswali makuu matatu yanayojirudia rudia kiasi cha kusababisha kero kwa Mtakatifu Petro! Daima anamuuliza ikiwa kama anampenda kuliko wengine wote! Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican, Ijumaa tarehe 2 Juni 2017.

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, Yesu anaamua kumdhaminisha Mtakatifu Petro wajibu wa kuwachunga kondoo wake! Petro mdhambi kuliko wadhambi wote miongoni mwa Mitume, huyu nditye aliyemkana Yesu mara tatu kwa kuapa kwamba, alikuwa hamfahamu hata chembe kidogo! Ndiyo maana Yesu anathubutu kumuuliza tena, ikiwa kama anampenda kuliko wengine wote? Anataka awachunge watu wake kwa fimbo ya upendo na wala si kwa kiburi wala jeuri; kwa kutawala na kuwagandamiza wengine.

Yesu akazia kwamba, hawa ni kondoo wake na Petro ni mdhamini tu, kumbe anapaswa kutenda kama wakili mwema, licha ya kutambua dhambi na mapungufu yanayowaandama kondoo wa Kristo ili kujenga na kudumisha urafiki kati yao! Petro anatambua fika kwamba, alimkana Yesu mara tatu na bado akilini mwake, anakumbuka imani yake kwa Kristo Yesu kuwa kweli Mwana wa Mungu aliye hai. Anatambua na kukumbuka, pale Yesu alipogeuka na kumwangalia, Petro, mtu mzima, akatiokwa na chozi la ibu na majonzi makuu kwa kumkana Yesu kwamba, halikuwa hamfahamu hata chembe kidogo! Petro, Mwamba, akakosa ujasiri kusimamia imani yake!

Baba Mtakatifu anakaza kusema, Mtume Petro alikuwa na ujasiri wa kumkana Yesu mbele ya watu akakumbana na aibu ya kulia kama mtoto mdogo na kuishi katika kutundikwa Msalabani, kama walivyomfanya Yesu, Petro Mtume, hana tena ile jeuri, bali amenyenyekeshwa na kuwa kama Mtumishi, ndiyo maana aliomba ateswe kichwa chini na miguu juu! Haya ndiyo waamini wanaweza kujifunza kutoka katika majadiliano ya Kristo Yes una Mtume Petro, majadiliano katika ukweli na uwazi; majadiliano yaliyofanyika katika hali ya utulivu kwa kugunda undani wa maisha ya mtu, kiasi cha kuleta mabadiliko makubwa katika maisha na utume wa Mtakatifu Petro, akatoka kimasomaso kumtangaza na kumshuhudia Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu!

Mwaliko kwa waamini ni kumwomba Mwenyezi Mungu, neema kama hii katika maisha yao, ili kulinda na kudumisha utu na heshima yao, kwa kutambua kwamba, daima dhambi iko mbele yao, lakini, Kristo Yesu ni mwingi wa huruma na mapendo, anataka kuwaokoa na kuwajalia utu mpya, tayari kutembea kifua mbele, ili kumtangaza na kumshuhudia kama alivyofanya Mtakatifu Petro!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.