2017-06-02 15:58:00

Marehemu Kardinali Husar alikuwa mwaminifu kwa Kristo na Kanisa lake!


Baba Mtakatifu Francisko amesikitishwa sana na taarifa za kifo cha Kardinali Lubomyr Husar, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo Katoliki la Kyiv-Halyc, Ukraine aliyefariki dunia, tarehe 31 Mei 2017 akiwa na umri wa miaka 84. Baba Mtakatifu katika salam zake za rambi rambi alizomwandikia Askofu mkuu Sviatoslav Shevchuk wa Jimbo Katoliki la Kyiv-Halyc anasema, anapenda kuungana na familia ya Mungu jimboni humo katika kuiombea roho ya Marehemu Kardinali Husar ili iweze kupata pumziko la milele na mwanga wa milele uweze kuiangazia. Ni kiongozi mashuhuri aliyejisadaka bila ya kujibakiza katika utume wake, ili kuweza kulipyaisha Kanisa nchini Ukraine.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, ni kiongozi aliyekuwa mwaminifu kwa Kristo na Kanisa lake, licha ya dhuluma na nyanyaso alizokumbana nazo katika maisha na utume wake. Alionesha moyo wa upendo na ubaba kwa ajili ya huduma ya kichungaji kwa familia zilizokuwa zimelazimishwa kuhamia Ukraine ya Magharibi. Alijielekeza zaidi na zaidi katika mchakato wa kukuza na kudumisha majadiliano ya kiekumene na Makanisa ya Kiorthodox. Baba Mtakatifu anapenda kwa namna ya pekee, kutoa salam zake za rambi rambi kwa wale wote walioguswa na msiba huu mzito, hasa ndugu na jamaa, wakleri na wale wote waliobahatika kupata huduma ya kichungaji kutoka kwa Marehemu Kardinali Husar. Baba Mtakatifu anapenda kuwapatia wote hawa baraka zake za kitume, akiwa na imani juu ya ufufuko wa wafu na uzima wa milele ijayo. Amina.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.