2017-05-31 09:13:00

Roho Mtakatifu katika maisha na utume wa Kanisa!


Kanisa linasadiki na kufundisha kuhusu Roho Mtakatifu, Bwana mleta uzima; atokaye kwa Baba na Mwana. Anayeabudiwa na kutukuzwa pamoja na Baba na Mwana: aliyenena kwa vinywa vya Manabii. Roho Mtakatifu anatenda pamoja na Baba na Mwana kama inavyojidhihirisha katika kazi ya uumbaji. Roho Mtakatifu anatawala, anatakatifuza na kuhuisha viumbe vyote. Roho Mtakatifu ameendelea kutenda kazi katika historia ya ukombozi wa mwanadamu unaofumbata Roho wa Kristo katika utimilifu wa nyakati. Kwa namna ya pekee kabisa, Roho Mtakatifu anaonekana katika Fumbo la Umwilisho, kwa kumwandaa Bikira Maria kuwa ni Tabernakulo ya kwanza ya Neno wa Mungu aliyefanyika mwili.

Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Padre Alcuin Nyirenda, OSB hivi karibuni wakati wa Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kuwapongeza wanafunzi watanzania waliopiga hatua katika madaraja mbali mbali ndani ya Kanisa, kwa baadhi yao kupewa Daraja la Ushemasi wa mpito unaofumbatwa katika huduma ya upendo na Neno kwa familia ya Mungu na Daraja ya Upadre inayowashirikisha dhamana ya kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Kuna baadhi ya watawa waliweka nadhiri katika hatua mbali mbali za safari ya wito wao kama watawa. Ilikuwa ni nafasi pia ya kuwaaga wanafunzi watanzania waliohitimu masomo yao kwa Mwaka 2016-2017, tayari kurejea tena Tanzania ili kujisadaka kwa ajili ya kuitumikia familia ya Mungu kwa ari, moyo mkuu, upole na unyenyekevu!

Padre Alcuin Nyirenda, OSB, anaendelea kufafanua akisema, Roho Mtakatifu alijionesha kwa namna ya pekee, Yesu alipokuwa anabatizwa Mtoni Yordani, wakat iwa mahubiri na miujiza yake, hadi pale alipoinama kichwa na kutoa Roho! Roho Mtakatifu ni paji la Mungu Baba! Yesu alipofufuka aliwaahidia wafuasi wake Ujio wa Roho Mtakatifu kwani kifo na ufufuko wake vilikuwa ni utimilifu wa ahadi ya Baba. Aliwaahidia Roho wa kweli, Msaidizi mwingine, atakayewafundisha, wakumbusha na kushuhudia yale yaliyotendwa na Kristo Yesu. Mwishoni, Yesu alitoa Roho yake kwa kuwavuvia wafuasi wake na tangu wakati ule utume wa Kristo na Roho Mtakatifu  unakuwa ni utume wa Kanisa: kama vile ”Baba alivyonituma Mimi, nami ninawatuma ninyi.”

Padre Alcuin Nyirenda, anasema katika mahubiri yake kwamba, mapaji yote saba ya Roho Mtakatifu yanapata utimilifu wote katika maisha na utume wa Yesu. Mapaji ya Roho Mtakatifu ni: Hekima, Akili, Shauri, Nguvu, Elimu, Ibada na Uchaji wa Mungu. Lakini anaonya kwamba, kutokana na Kristo Yesu kujinyenyekesha na kuwa sawa na binadamu katika mambo yote isipokuwa dhambi, kuna hatari ya mazoea na dharau kuanza kuingia katika maisha ya waamini! Badala ya kukuza na kudumisha ibada na uchaji wa Mungu, maeneo matakatifu yanakuwa sasa ni mahali pa michapo! Badala ya kumwogopa Yesu, sasa waaamini wanapoingia Kanisa, wanamtisha hata Yesu mwenyewe! Hii ni hatari ambayo kila mwamini wakati huu, Kanisa linapongojea utimilifu wa ahadi ya Mungu, kujichunguza ndani mwake, ili kufanya toba na wongofu wa ndani, tayari kumkaribisha Roho Mtakatifu atakayewasaidia kuwafundisha na kuwakumbusha mambo msingi yanayofundishwa na Kristo Yesu katika maisha yake, tayari kuyashuhudia kama kielelezo cha imani tendaji!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.