2017-05-28 13:44:00

Wosia wa Baba Mtakatifu Francisko kwa vijana wa kizazi kipya!


Vijana wanapaswa kuwa ni mashuhuda na vyombo vya furaha ya Injili ya imani, matumaini, mapendo na mshikamano miongoni mwa vijana wenzao wanaotumbukizwa katika biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya; mifumo ya utumwa mamboleo, fujo na vurugu za maisha ya ujana. Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana ni fursa makini kwa Mama Kanisa kusikiliza matamanio halali ya vijana na kuyapatia majibu muafaka. Kanisa linataka kuandamana na vijana katika hija ya maisha yao, ili kuwajengea uwezo wa kufanya maamuzi magumu katika maisha.

Ni wajibu wao kujenga utamaduni wa sala, tafakari ya Neno la Mungu, upendo na mshikamano na vijana wenzao pasi na ubaguzi. Wawe makini katika mchakato wa ujenzi wa Injili ya upendo itakayowasaidia kuunda familia, Kanisa dogo la nyumbani! Mahusiano haya hayana budi kuwa kweli makini, yenye utimilifu na yanayojikita katika uaminifu. Vijana hata katika ujana wao, wanahamasishwa na Mama Kanisa kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa mshikamano wa upendo na wahamiaji pamoja na wakimbizi wanaotafuta hifadhi, usalama na maisha bora zaidi!

Hizi ni dukuduku zilizoibuliwa na vijana wakati Baba Mtakatifu Francisko alipokutana na kuzungumza na vijana uso kwa uso kutoka ndani na nje ya Jimbo kuu la Genova, Jumamosi, tarehe 27 Mei 2017. Baba Mtakatifu anawataka vijana kuwa ni vyombo na mashuhuda wa utimilifu wa furaha inayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake. Wajifunze kuwa ni wamissionari wanaochota utajiri unaofumbatwa katika tunu msingi za maisha ya kifamilia, vyama vya kitume na Kanisa katika ujumla wake, tayari kuwafunguliwa wengine hazina ya akili na mioyo yao; watu makini wanaowajibika katika maboresho ya maisha yao, wakiwa na malengo thabiti, kamwe wasiwe ni watalii katika hija ya maisha yao hapa duniani.

Baba Mtakatifu anawataka vijana kuondokana na tabia ya unafiki, daima wawe wakweli na wa wazi katika kufikiri na kutenda, tayari kushiriki katika maisha na utume wa Kanisa; kwa kuisikiliza sauti ya Yesu anayewaita na kuwatuma kuwa ni mashuhuda wa furaha ya Injili. Wajitahidi kukutana na Kristo Yesu katika maisha yao, ili awaguse, awagange na kuwaponya kutoka katika shida na mahangaiko yao, kama alivyofanya kwa yule mwanamke aliyekuwa anatokwa damu kwa muda wa miaka kumi na miwili. Vijana watambue na kuthamini kwamba,  wao wote ni ndugu katika Kristo kwani wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Vijana ni sehemu ya Kanisa moja, takatifu, katoliki na la mitume! Kanisa linaloundwa na wadhambi wanaojitaabisha kutubu, kuongoka na kuchuchumilia utakatifu wa maisha.

Vijana wakitaka kuwa kweli ni wamissionari makini miongoni mwa vijana wenzao wa kizazi kipya wanapaswa kwanza kabisa kuwapenda na kuwathamini, tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya maisha yao kiroho na kimwili! Kupenda na kujiaminisha kwa jirani, ili kushiriki katika furaha, mateso na matumaini yao. Vijana wawe ni vyombo vya Injili ya matumaini kwa wale wanaotumbukizwa kwenye biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya, vijana wanaonyanyaswa na kudhulumiwa utu na heshima yao kutokana na mifumo mbali mbali ya utumwa mamboleo, vita, kinzani na mipasuko ya kijamii!

Wote hawa anasema Baba Mtakatifu Francisko, wanapaswa kutangaziwa na kushuhudiwa Injili ya matumaini, kwa kujifunza kuangalia na kupenda kwa jicho la Kristo Yesu, lakini kwa namna ya pekee kwa kuzama katika Moyo wake Mtakatifu, chemchemi ya huruma na mapendo kwa binadamu! Injili ya matumaini inapaswa kuwagusa wote hasa wale waliokata tamaa katika maisha, ili kwa njia ya uwepo wao, wamwone Kristo Yesu, Mkombozi wa ulimwengu, anayewasubiri ili kuwaganga na kuwatakasa, tayari kuanza kuandika upya kurasa za historia ya maisha yao! Vijana wawe ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya upendo, huruma na msamaha, ili kuondokana na utamaduni wa utupu na upweke wa maisha, tayari kujenga na kudumisha umoja, udugu, upendo na mshikamano bila kumtenga mtu awaye yote!

Baba Mtakatifu Francisko anaikumbusha familia ya Mungu Genova kwamba, imefumbatwa katika ukarimu, ujasiri na mwono mpana kwani hii ni familia ambayo imezungukwa na bahari. Maendeleo ya sayansi na teknolojia, yawawezeshe vijana kuwa na upeo mpana wa mambo ili kupambana na changamoto za maisha. Wawe na ujasiri wa kumwomba Yesu ili awajengee uwezo wa kutafuta kilicho kweli, chema na cha haki. Wasikubali kupewa majibu mepesi mepesi katika maisha kwa kutafuta njia ya mkato kwani matokeo yake ni kutumbukizwa katika biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya!

Vijana wanatakiwa kujenga umoja, udugu na urafiki na kamwe wasiwapatie jirani na wenzi wao kisogo, kwani hizi ni dalili za ubinafsi. Waoneshe moyo wa ukarimu na mapendo kwa wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta usalama, hifadhi pengine na maisha bora zaidi. Ni watu wanaokabiliana na kifo kila siku ya maisha yao, kiasi kwamba, Bahari ya Mediterrania imegeuka kuwa ni kaburi lisilo na alama, kuna maelfu ya watu waliomezwa kwenye tumbo la bahari na kusahaulika kutokana na ubinafsi.

Baba Mtakatifu anachukua fursa hii kuzipongeza nchi zile ambazo zimeonesha wema na ukarimu kwa wakimbizi na wahamiaji na kwa namna ya pekee, Italia ambayo imekuwa ni kituo cha matumaini ya wakimbizi na wahamiaji wengi! Duniani kuna watu wanakufa kwa baa la njaa, ujinga na maradhi; kuna watu wanadhulumiwa na kunyanyaswa utu na heshima yao kutokana na biashara haramu ya binadamu. Kuna watu ambao mtutu wa bunduki umekuwa ni chakula chao cha kila siku! Ili kuwapokea na kuwakirimia watu wa namna hii, kunahitajika ujasiri na ukarimu wa Kiinjili.

Watu kama Nahodha Cristoforo Colombo walikuwa na ujasiri wa kupambana na changamoto za maisha! Vijana waombe ujasiri kama huu kutoka kwa Kristo Yesu, ili waweze kweli kupambana changamoto zinazowakabili kila siku ya maisha yao! Mwishoni, Baba Mtakatifu amehitimisha majadiliano yake na vijana kutoka ndani na nje ya Genova kwa baraka kwa ajili ya wafunga kutoka Genova na Liguria waliokuwa wanafuatilia majadiliano yake na vijana na baadaye kuelekea katika ukumbi maalum kwa ajili ya kupata chakula cha mchana na maskini, wafungwa, wakimbizi na wahamiaji! Wote hawa wameonjeshwa furaha ya Injili na matumaini yanayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu na Kanisa lake!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.