2017-05-28 14:19:00

Vigezo msingi katika utekelezaji wa maisha ya kipadre na kitawa!


Baba Mtakatifu Francisko akiwa Jimbo kuu la Genova, Jumamosi, tarehe 27 Mei 2017 amekutana na kuzungumza na: wakleri, watawa na majandokasisi kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Lorenzo. Baba Mtakatifu amefafanua kwa kina na mapana juu ya vigezo vinavyopaswa kutumiwa na wakleri katika kutekeleza dhamana, majukumu na utume wao katika ulimwengu mamboleo, unaoonekana kuwapeleka mchaka mchaka! Umoja na udugu wa maisha na utume wa Kipadre unarutubishwa kwa njia mikutano, hija za maisha ya kiroho, mafungo pamoja na ujirani mwema, lakini Baba Mtakatifu amekazia zaidi huduma na mshikamano na maskini! Amewataka watawa kuhakikisha kwamba, wanaishi kwa uaminifu karama na utume wao kama sehemu ya utekelezaji wa sera na mikakati ya kichungaji jimboni mwao! Mwishoni, amegusia changamoto ya kukauka kwa miito ya kipadre na kitawa Barani Ulaya!

Baba Mtakatifu anasema, mtindo na mfumo wa Kristo Yesu unaonesha kwamba, daima alikuwa ni mtu aliyetembea ili kukutana na kuwasikiliza watu wa kila aina na kuwapatia majibu muafaka ili kuzima kiu ya maisha yao ya ndani. Kwa njia hii, Yesu alikuwa karibu pamoja na watu; akatambua matatizo, changamoto na fursa zao na kuzipatia majibu muafaka. Daima alijitahidi kuanza na kuhitimisha matukio makubwa katika maisha yake kwa njia ya sala. Wakleri na watawa wanapaswa kutekeleza majukumu yao kwa utulivu bila haraka kwani haraka haraka haina baraka. Wawe ni watu wa kusoma alama za nyakati na kamwe wasiwe ni watumwa wa muda. Wajitahidi kuadhimisha mafumbo ya Kanisa kwa ibada na uchaji na kamwe si kama wafanyakazi wa mshahara. Wawe ni mahujaji, wazi na tayari kupokea maajabu yanayoletwa na Mwenyezi Mungu katika maisha yao. Maisha na wito wa kipadre na kitawa daima ni mapambano endelevu yanayopaswa kusimikwa katika sala na tafakari ya Neno la Mungu; katika huduma makini na shirikishi!

Yesu katika maisha yake alikutana na wagonjwa, maskini, waliopagawa na wadhambi. Mapadre wajitahidi kukutana na Kristo Yesu katika Fumbo la Ekaristi Takatifu na Mwenyezi Mungu katika sala na waamini katika huduma. Mapadre na watawa wajenge sanaa ya kusikiliza kwa makini shida na mahangaiko ya watu! Wajitahidi kukutana na Kristo mfufuka miongoni mwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Wajenge moyo wa saburi na uvumilivu, daima wakijikita katika kipaji cha ubunifu, sadaka na utayari, vinginevyo, watachoka na kuwachosha waamini wao. Wawe na jicho la huruma na mapendo kwa wale wanaotaka huduma yao; hao ndio pia wanaowasindikiza katika maisha na utume wao kwa sala, sadaka na majitoleo yao.

Baba Mtakatifu anawaonya mapadre na watawa kuhusu tabia ya kujitafuta wenyewe; kutafuta ”ujiko” na umaarufu usiokuwa na tija wala mashiko; hizi ni dalili za utupu katika maisha. Mapadre na watawa wawe ni watu wa sala, tafakari makini ya Neno la Mungu; hata katika mchoko waoneshe uvumilivu, ari na moyo mkuu, kwani hizi ni cheche za utakatifu wa maisha. Wawe ni madaraja ya kukutana na watu; kielelezo cha ibada ya kuabudu Ekaristi Takatifu; wahudumu wa familia ya Mungu wanaoweza kusikiliza kwa makini; wanaowaheshimu na kuwathamini jirani zao, tayari kushiriki katika maisha na utume wa Kanisa kwa furaha na uaminifu mkubwa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.